
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Hamida Mussa Khamis Shuduma, amesema ameridhishwa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), hususan huduma ya Certificate of Origin, akisema ni nyenzo muhimu katika kukuza biashara na kuimarisha uchumi wa wananchi.
Mhe. Hamida ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea banda la TNCC katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar (Zanzibar International Trade Fair – ZITF), ambapo alisema huduma ya Certificate of Origin inawasaidia wafanyabiashara kurahisisha shughuli za biashara za kimataifa na kufungua fursa mpya za masoko ya nje.
Amesisitiza kuwa huduma hiyo ina mchango mkubwa katika kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kikanda na kimataifa, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya TNCC, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Bw. Matina Nkurlu, amesema taasisi hiyo itaendelea kujikita katika kutoa huduma zenye tija kwa wafanyabiashara, ikiwemo huduma ya Certificate of Origin ambayo imekuwa chachu ya kuwawezesha wajasiriamali wa Kitanzania kupanua wigo wa masoko yao nje ya nchi.
Bw. Nkurlu ameongeza kuwa TNCC inaendelea kuboresha huduma zake ili kuhakikisha wafanyabiashara wengi zaidi wanapata taarifa sahihi na msaada unaohitajika katika kuendeleza biashara zao.




Toa Maoni Yako:
0 comments: