Dar es Salaam, Tanzania – Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa kushirikiana na huduma za usafiri za Bolt wamezindua ushirikiano maalum unaolenga kuwahamasisha Watanzania kufanya maamuzi salama baada ya kusherehekea, hasa katika kipindi cha sikukuu ambapo ajali zinazohusiana na ulevi huongezeka.

Ushirikiano huu, uliozinduliwa jijini Dar es Salaam, unaunganisha kampeni ya unywaji wa kuwajibika ya SBL inayojulikana kama Wrong Side of the Road (WSOTR) na huduma za Bolt, ili kuhakikisha usafiri salama upo rahisi kupatikana kwa Watanzania. Mpango huu unalenga kuhakikisha wananchi wanafurahia sherehe zao huku wakirudi nyumbani salama, hususan katika kipindi chenye msongamano mkubwa wa magari barabarani.

Disemba kwa kawaida ni mwezi wenye shughuli nyingi za barabarani kutokana na safari nyingi, mikusanyiko ya kijamii na unywaji wa pombe. Changamoto hii mara nyingi huongeza hatari za ajali za barabarani. Kupitia ushirikiano huu, SBL na Bolt wanahamasisha Watanzania kuacha magari yao na kutumia usafiri salama baada ya kunywa, hivyo kupunguza hatari.
Kampeni ya Wrong Side of the Road, iliyoanzishwa mwaka 2023 na kuendelea kuboreshwa chini ya kaulimbiu ya Inawezekana Kabisa – Sherehe Salama, Nyumbani Salama, inalenga kupunguza ajali zinazohusiana na unywaji wa pombe na kuhimiza maamuzi sahihi. Kwa mfano, wananchi watakaotazama video ya elimu ya kampeni na kupata cheti chao watapokea Sherehe Code, inayowapa punguzo la 30% kwa safari za Bolt katika kipindi chote cha sikukuu. Aidha, kila safari inatoa nafasi ya kuchaguliwa kupanda Special Bolt, gari maalum lenye muonekano wa kipekee wa sikukuu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Meneja Mawasiliano na Uendelevu wa SBL, Rispa Hatibu, alisema ushirikiano huu unaonyesha dhamira ya kampuni kwa jamii inayozihudumia.
“Disemba ni kipindi cha sherehe kubwa kwa Watanzania, lakini hakuna sherehe inayopaswa kuishia katika majonzi. Kupitia ushirikiano huu na Bolt, tunawahimiza watu kufurahia kwa kuwajibikaji na kufanya maamuzi salama ya namna ya kurudi nyumbani,” alisema Hatibu.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Bolt kwa Tanzania, Kenya na Uganda, Dimmy Kanyankole, alisema mpango huu unarahisisha upatikanaji wa usafiri salama katika kipindi chenye msongamano mkubwa wa safari.

“Lengo letu ni kuondoa vikwazo vya usafiri salama kwa kufanya iwe rahisi, nafuu na ipatikane pale inapohitajika zaidi,” alisema Kanyankole.

Kampeni hii itaendeshwa katika kipindi chote cha sikukuu, ikianzia katika maeneo makubwa ya burudani na maisha ya usiku jijini Dar es Salaam, kabla ya kupanuliwa mikoa mingine nchini. SBL na Bolt wamesisitiza kuwa ujumbe wa kampeni ni rahisi: Watanzania hawalazimiki kuchagua kati ya kusherehekea na kurudi nyumbani salama. Inawezekana Kabisa kufanya yote mawili.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: