Dodoma, Desemba 17, 2025: Serikali ya Marekani imetangaza kuiweka Tanzania katika kundi la nchi zilizoanza kudhibitiwa kwa taratibu za visa za kuingia nchini humo, hatua iliyotokana na viwango vya juu vya raia wanaokiuka masharti ya visa, hususan kwa kuzidisha muda wa ukaaji.Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, uamuzi huo ulitangazwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, tarehe 16 Desemba 2025, na unahusisha jumla ya nchi 15, zikiwemo pia baadhi ya nchi za Afrika.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Tanzania ina viwango vya ukaaji wa zaidi ya muda unaoruhusiwa vya asilimia 8.30 kwa visa za B1/B2 (biashara na utalii) na asilimia 13.97 kwa visa za F, M na J zinazohusisha wanafunzi, mafunzo ya ufundi na programu za kubadilishana.
Kutokana na viwango hivyo, Serikali ya Marekani imeeleza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda mifumo yake ya uhamiaji na kuhakikisha kuwa waombaji wa visa wanazingatia kikamilifu masharti wanayopewa.
Hata hivyo, Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa vikwazo hivyo si marufuku kamili, bali ni udhibiti wa taratibu za utoaji visa, na kwamba Watanzania wanaokidhi vigezo na masharti wataendelea kupewa visa kulingana na tathmini itakayofanywa.
Serikali imesema itaendelea kufanya mazungumzo ya kidiplomasia na Serikali ya Marekani ili kufikia muafaka kwa maslahi ya wananchi, huku ikiwasisitiza Watanzania wanaosafiri kwenda Marekani kuzingatia kikamilifu masharti ya visa ili kuepuka athari binafsi na kwa taifa kwa ujumla.
Wizara ya Mambo ya Nje imesisitiza kuwa itaendelea kutoa taarifa kadri mazungumzo na hatua zaidi zitakavyoendelea.


Toa Maoni Yako:
0 comments: