Blantyre, Septemba 27, 2025: Rais mteule wa Malawi, Profesa Arthur Peter Mutharika, amewataka wananchi wote wa nchi hiyo kuungana na kushirikiana katika kujenga taifa, akisisitiza kuwa kipindi cha ushindani wa kisiasa kimekwisha na sasa ni wakati wa kuwaletea maendeleo wananchi.

Akihutubia taifa kwa mara ya kwanza kutoka nyumbani kwake mjini Blantyre tangu atangazwe mshindi wa uchaguzi, Prof. Mutharika alisema:

"Uchaguzi huu umeisha. Ushindani umeisha. Sasa ni wakati wa kuungana na kuwatumikia wananchi wetu," akitoa mkono wa ushirikiano kwa Wamalawi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa.

Rais mteule pia aliipongeza Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) kwa kuendesha mchakato wa uchaguzi kwa weledi na uwazi, hatua iliyosifiwa ndani na nje ya nchi kwa kuimarisha uhalali wa matokeo.

Hata hivyo, Prof. Mutharika alionyesha msimamo mkali dhidi ya vitendo vya rushwa na uzembe katika utumishi wa umma, akionya watumishi wa serikali wanaojihusisha na vitendo vya hila kuacha mara moja.

"Serikali yangu haitavumilia ufisadi wala vitendo vya udanganyifu," alionya.

Kwa ujumla, hotuba ya Prof. Mutharika imeashiria mwelekeo wa kuunganisha taifa lililokuwa limegawanyika wakati wa kampeni za uchaguzi, na kutoa matumaini mapya ya mshikamano wa kitaifa na mageuzi ya kijamii na kiuchumi katika awamu mpya ya uongozi wake.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: