Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Dodoma, Agosti 8, 2025 – Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza rasmi ratiba ya kuchukua fomu za uteuzi kwa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka vyama 14 vya siasa, ambapo mchakato huo utaanza kesho, Agosti 9, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa INEC, Ndugu Kailima Ramadhani, amesema kuwa hadi kufikia leo, Tume imepokea barua kutoka vyama hivyo 14 zenye kuainisha tarehe na muda wa wanachama wao waliopendekezwa kwa nafasi hizo kufika ofisi za Tume zilizopo Njedengwa kwa ajili ya kuchukua fomu za uteuzi.

“Tarehe 09 Agosti, wagombea kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), National Reconstruction Alliance (NRA) na Alliance for African Farmers Party (AAFP) watakuwa wa kwanza kuchukua fomu za uteuzi,” amesema Ndugu Kailima.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, tarehe nyingine za kuchukua fomu ni kama ifuatavyo:

● 10 Agosti, 2025: Chama cha MAKINI, The National League for Democracy (NLD), na United Peoples’ Democratic Party (UPDP)

● 11 Agosti, 2025: African Democratic Alliance Party (ADA – TADEA), Union for Multiparty Democracy (UMD), na Tanzania Labour Party (TLP)

● 12 Agosti, 2025: Chama Cha Kijamii (CCK), Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), na Alliance for Democratic Change (ADC)

● 13 Agosti, 2025: Democratic Party (DP)

● 15 Agosti, 2025: National Convention for Construction and Reform (NCCR – MAGEUZI)

Ndugu Kailima amefafanua kuwa ratiba hiyo ni kwa vyama vilivyowasilisha taarifa zao hadi leo na iwapo kutakuwepo na vyama vingine vitakavyowasilisha taarifa zao baadaye, Tume itaandaa na kutangaza ratiba nyingine.

“Tunavipongeza vyama vyote kwa hatua ya maandalizi inayoendelea kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Tume itaendelea kuhakikisha kuwa mchakato mzima unazingatia Katiba, Sheria na Kanuni,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa INEC, hatua ya kuchukua fomu ni miongoni mwa hatua muhimu za kisheria kuelekea uchaguzi mkuu, ambapo baada ya uchukuaji wa fomu, wagombea watatakiwa kurejesha kwa mujibu wa taratibu zilizoainishwa.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: