• Yamaliza mwaka kwa ongezeko la wateja asilimia 16.9 na kufikia milioni19.6, na ongezeko la asilimia 15.1 kwa watumiaji wa data hivyo kufikia wateja milioni 10.1.
• Imewekeza katika miundombinu ya mtandao inayoharakisha usambazaji wa teknolojia ya 4G na 5G, huku pia ikiboresha miundombinu ya TEHAMA.

• Imechangia vyema katika kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuziba mgawanyiko wa kidijitali kupitia maboresho ya huduma ya M-Pesa na huduma bunifu za kidijiti katika sekta muhimu.

Dar es Salaam - Septemba 11, 2024: Kampuni inayoongoza kwa teknolojia na mawasiliano nchini Vodacom Tanzania PLC, leo imefanya mkutano mkuu wa mwaka ambapo ripoti jumuishi ya mwaka kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 31 Machi 2024 iliwasilishwa kwa wanahisa. Ripoti hiyo inatoa muhtasari wa mwenendo wa biashara na mazingira ya uendeshaji wa kampuni hiyo pamoja na kuhakiki mkakati wake, utendaji na utawala kwa mwaka wa fedha ulioishia mwezi Machi mwaka huu.

Katika wasilisho lake kwa wanahisa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Vodacom Tanzania Plc Jaji Mstaafu Thomas Mihayo, alieleza kwa undani mazingira ya uendeshaji kwa mwaka uliopita Pamoja na uimara wa kampuni hiyo umeiwezesha Vodacom kudumisha nafasi yake ya uongozi katika soko na huku wateja wakionesha kuridhika kupitia maoni yaliyopimwa na kipimo kiitwacho Net Promoter Score (NPS).

"Uwekezaji wetu katika miundombinu na huduma mbalimbali za kibunifu umeimarishwa na mazingira bora ya kisera, biashara pamoja na udhibiti. Kuondolewa kwa ushuru kwa miamala ya pesa za simu wakati wa kutuma baina ya wateja ni mfano muhimu wa mabadiliko haya chanya. Zaidi ya hayo, uwezo wetu wa kukua na kuongeza thamani umechangiwa na wadau wetu wote pamoja na wateja wetu. Hili linathibitishwa na nafasi yetu ya kuongoza katika alama za Net Promoter Score, huku tukimaliza mwaka tukiongoza kwa tarakimu maradufu dhidi ya mshindani wetu wa karibu zaidi,” alisema Jaji Mihayo.

Ripoti ya kila mwaka ya Vodacom inaonyesha kuwa utendaji wa kifedha wa kampuni umeongezeka, huku ukuaji wa EBITDA (Mapato kabla ya riba, kodi, kushuka kwa thamani na upunguzaji wa madeni) ukikaribia asilimia 20, hii ilisaidia ongezeko la asilimia 65 ya faida ya uendeshaji na faida halisi baada ya kodi ya Shilingi bilioni 53.4.

"Mafanikio haya yametokana na mpango wetu wa kina wa uboreshaji wa gharama, ambao ulitekelezwa bila kuathiri viwango vya huduma kwa wateja au uwekezaji. Kwa kuzingatia ufanisi huu wa kifedha, Bodi imeidhinisha gawio la Shilingi 11.93 kwa kila hisa ambayo imetokana na asilimia 50 ya faida yetu baada ya kodi kulingana na muongozo wa sera yetu ya gawio. Kwa niaba ya Bodi, natoa shukrani zetu za pamoja kwa uongozi wa Vodacom, wafanyakazi, na washirika wa kibiashara kwa mchango wao katika ufanisi wa mwaka huu,” alihitimisha Jaji Mihayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Philip Besiimire alisema kwamba matokeo mazuri ya kifedha, yameletwa na uthabiti na utekelezaji wa mkakati wa kampuni hiyo, ulioungwa mkono na mazingira mazuri ya kisera, kuondolewa kwa tozo ya kutuma miamala baina ya wateja, pamoja na kupunguzwa kwa ada zinazolipwa ili kutumia miundombinu ya mawasiliano (right of way fees), sera za serikali za kuunga mkono uwekezaji kwa sekta kibinafsi, pamoja na uwekezaji mkubwa wa umma.

"Kupitia wateja milioni 10 wa M-Pesa, tumeendelea kuongoza soko na tukiwa na asilimia 30.5 ya wateja wa pesa kupitia simu za mkononi, hii ikisukumwa na adhma yetu ya kumuweka mteja kwanza siku zote. Zaidi ya hayo, M-Pesa ilionyesha ukuaji zaidi kwa mwaka huu ambapo kumekuwa na ongezeko la asilimia 27.8 la mapato, na kupanda hadi asilimia 36 kwa jumla ya miamala iliyofanywa. Tumemaliza mwaka kwa ongezeko la asilimia 16.9 ya wateja wetu kwa ujumla na kufikia milioni 19.6. Kadhalika, kulekuwa na ongezeko la asilimia 15.1 la watumiaji wa data hadi kufikia wateja milioni 10.1,” alisema Besiimire.
Kwa kuzingatia madhumuni ya kampuni ya 'kuunganishwa kwa maisha bora ya baadaye' na dhamira yake ya kupunguza mgawanyiko wa kidijitali nchini, Vodacom iliwekeza shilingi bilioni 170.1 katika kupanua wigo na uwezo wa mtandao, kuharakisha usambazaji wa 4G na 5G pamoja na miundombinu ya Tehama. Uwekezaji huu unalenga kuboresha viwango vya huduma kwa wateja, kuimarisha usalama wa mtandao na kutumia fursa katika sehemu ambazo hazijapenyezwa sana kama vile kuleta suluhu za IoT (Internet of Things).

Besiimire alisisitiza zaidi kuwa mnamo mwezi Machi Mwaka huu, Vodacom Tanzania ilikamilisha ununuzi wa kampuni ya Smile Communications Tanzania Limited, hii iliiwezesha Vodacom kupata masafa muhimu ya 800MHz na 2600MHz. Hii itaboresha kwa kiasi kikubwa miundombinu ya mtandao wa kampuni na hivyo kuboresha huduma kwa wateja.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji alibainisha kuwa kampuni hiyo iliboresha madhumuni yake na hivyo kuzingatia "kuiwezesha jamii" na "kuilinda sayari" katika jamii ya kidijitali. Juhudi za Vodacom kama vile m-mama kwa ajili ya afya ya uzazi, Code like a Girl, maendeleo ya uongozi wa wanawake na harakati za upandaji miti, zinaonyesha kujitolea kwa kampuni hiyo katika kuleta jamii endelevu na jumuishi ya kidijitali.
"Jukwaa letu la M-Kulima linaunganisha wakulima wadogo zaidi ya milioni 3 kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, kutoa taarifa muhimu na kuwezesha malipo salama kupitia M-Pesa. Zaidi ya hayo, mradi wetu mpya wa kubadilisha nishati unapunguza kiwango cha kaboni, kwa kuzingatia lengo la Vodacom Group la kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2035,” alifafanua Besiimire.

Mkurugenzi Mtendaji alisisitiza kwamba kampuni hiyo inakusudia kutoa huduma zenye ubora wa hali ya juu kwa wadau wote haswa wanapoangalia idadi ya vijana inayoongezeka nchini, pamoja na upenyaji mdogo wa dijitali ambao unatoa fursa za ukuaji katika nyanja hiyo. Pia aliongeza kuwa Vodacom imejipanga vyema kutumia fursa hizi ikiwa ni kampuni inayoongoza katika eneo la FinTech.

Kwa kumalizia, Besiimire alihakikisha kwamba licha ya kuwa na mazingira yanayotia shaka ya kijiografia (geopolitical environment) na changamoto za ndani kama vile upatikanaji wa fedha za kigeni, Vodacom inasisitiza nia ya kuleta thamani endelevu kwa wanahisa wake wote pamoja na jumuiya yote ya washikadau, huku ikisukumwa na umakini wa kampuni katika wateja, urahisi na ukuaji.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: