Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania-TANAPA kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imeanza kutoa Anwani za Makazi katika kambi, makazi, hoteli na vivutio vya utalii katika maeneo ya Hifadhi zake zote 21.

Zoezi hilo ambalo litafanyika kwa awamu linaenda sambamba na kusajili taarifa za Anwani za Makazi katika Mfumo wa Kidigitali unaojulikana kwa jina la NaPA, hatua inayolenga kuboresha shughuli za utalii katika hifadhi hizo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo kwa mazungumzo na makubaliano baina ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambayo ni Mratibu wa Utekelezaji na Matumizi ya Mfumo; Wizara ya Maliasili na Utalii na TANAPA.

Akitoa tamko la kuanza kutoa na kusajili Anwani za Makazi katika Hifadhi hizo, leo tarehe 27 Agosti, 2024, Naibu Kamishna wa Uhifadhi - Maendeleo ya Biashara wa TANAPA, Kamishna Massana Mwishawa amesema lengo ni kurahisisha shughuli za utalii hususan kuwawezesha watalii kufika maeneo mbalimbali ya utalii kwa urahisi.

Kamishna Mwishawa ambaye alimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Bw. Juma Kuji, amesema utoaji na usajili wa Anwani za Makazi litaanzia na Hifadhi na mbuga tatu zilizo ndani ya Mikoa ya Arusha na Manyara ambazo ni Hifadhi ya Taifa Arusha, Hifadhi ya Taifa Tarangire na Hifadhi ya Taifa Manyara.
Mratibu wa Anwani za Makazi Taifa, kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Jampyon Mbugi ameipongeza TANAPA kwa utayari wao wa kutumia Mfumo katika kuboresha huduma za utalii.

Amesema kuwa, Mfumo wa Anwani za Makazi ni Mfumo wa Utambuzi ambao pamoja na masuala mengine utachochea jitihada zilizoanzishwa na Serikali katika kutangaza utalii na kwamba utatumiwa na Sekta zote za Kijamii na Kiuchumi zikiwemo za utalii, biashara, ulinzi, usalama na uokoaji.

Awali wakiwasilisha mada kuhusu mfumo huo unavyotumika na faida zake mbele ya Menejimenti ya TANAPA, wataalamu wa Mfumo huo kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wameainisha faida ambazo TANAPA itazipata kwa hifadhi zake kutambuliwa na mfumo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: