Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha SAGCOT, kinachoratibu maendeleo ya kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Ukuaji wa Kilimo Tanzania (SAGCOT),Geoffrey Kirenga amesema watamkumbuka Rais wa awamu ya Pili, Ali Hassan mwinyi kwa kuleta ushawishi mkubwa katika maendeleo ya kilimo nchini.

Kauli hiyo ameitoa katika taarifa yake ya buriani kwa Rais huyo aliyezikwa kijini kwao Mangapwani kisiwani Unguja Machi 2 mwaka huu.

Alisema kifo Rais Mwinyi, aliyeliongoza taifa la Tanzania kuanzia mwaka 1985 hadi 1995 ni pigo kubwa kwa wakulima na wadau wa maendekeo kwa ujumla.

"Kipindi cha Rais Mwinyi kilikuwa alama ya sera za mageuzi zilizoboresha kilimo, nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania na ustawi wa wananchi wake," Kirenga alisema.

Alisema chini ya uongozi wa Mwinyi, nchi ilianza Mpango wa Urekebishaji wa Uchumi mnamo mwaka 1986, hatua muhimu iliyolenga utulivu wa uchumi na marekebisho ya kimiundombinu yaliyohamasisha biashara binafsi na kurahisisha vizuizi vya uagizaji.

"Juhudi zake zilikuwa muhimu katika kujihusisha tena na taasisi za fedha za kimataifa kama Benki ya Dunia na IMF, hivyo kuiwezesha Tanzania kutoka katika matatizo ya kiuchumi na kuelekea kwenye njia ya ustawi," Kirenga alifafanua zaidi.

Utawala wa Mwinyi pia unakumbukwa kwa kuanzisha mfumo wa vyama vingi, ukianzisha enzi mpya wa kiuchumi na mageuzi ya kisiasa. Licha ya kukabiliwa na changamoto kama vile migogoro ya kifedha, ukame, na athari za mshtuko wa bei ya mafuta duniani, sera za Mwinyi ziliielekeza Tanzania kuelekea uchumi unaotegemea soko, zikibadilisha mwelekeo wa baadaye wa nchi.

"Katika miaka yake ya mwisho, Rais Mwinyi alijishughulisha kwa dhati na kilimo, akihamasisha faida za kilimo kwa vijana wa Tanzania. Shamba lake la papai huko Msalato, Dodoma, linasimama kama ushuhuda wa imani yake katika kilimo kama chachu ya maendeleo," alisema Kirenga.

Utetezi huu unaendana na juhudi za Rais wa sasa, Samia Suluhu Hassan, hususan Agenda 10/30 na Mipango Mkuu wa Mabadiliko ya Kilimo, yenye lengo la kuiinua sekta ya kilimo ya Tanzania hadi mafanikio mapya ifikapo mwaka 2030.

Kupitia urithi wake, Ali Hassan Mwinyi , Kirenga anasema anaendelea kuhamasisha vizazi vijavyo na mipango yenye lengo la kubadilisha sekta ya kilimo ya Tanzania, kuhakikisha mustakabali wenye ustawi na endelevu kwa taifa na wananchi wake.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: