Kuelekea kumbukumbu ya kumuenzi baba wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alifariki Oktoba 14, 1999, msafara wa waendesha baiskeli unaojulikana kama Twende Butiama umeanza rasmi safari leo katika makazi yake Msasani jijini Dar es Salaam ambapo unatarajiwa kufikia tamati Oktoba 14, Wilayani Butiama.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Meneja Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa, Bw. Benson Chacha aliwapongeza waandaaji wa Twende Butiama pamoja na wadhamini wa msafara huo, taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kwa jitihada za kufanikisha tukio hili ambalo linahamasisha Watanzania kupenda michezo, kutunza mazingira na kujali afya zao.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa dhati waandaji na washiriki wote wa msafara wa Twende Butiama ambao wana dhamira ya dhati ya kumuenzi baba wa taifa. Tukio hili sio tu linachagiza shughuli mbalimbali ambazo Mwalimu Nyerere alikuwa anazipa kipaumbele lakini pia zitahamasisha Watanzania kupenda michezo. Michezo ni sekta muhimu ambayo ukiachana na kuimarisha afya lakini pia huleta umoja na mshikamano miongoni mwa watu. Pia, niwapongeze Vodacom kwa kudhamini ziara hii ambayo itapita mikoa tofauti ukihamasisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Mchango wenu kwenye kudhamini sekta ya michezo tunaufahamu na tungependa kuona mkifanya hivyo kwenye michezo mingine kama vile riadha, masumbwi, na kadhalika,” alimalizia Bw. Chacha.

Madhumuni ya msafara huu utakaokuwa na waendesha baiskeli takribani 200 watakaoendesha baiskeli kwa kilometa 1,500 na kupita kwenye wilaya 20 ndani ya mikoa 10, ni kuenzi maisha na urithi aliotuachia Mwalimu Nyerere ambapo alikuwa akipambania kuhusu elimu bora, upatikanaji wa huduma za afya ili kuondokana na maradhi pamoja na ukuaji wa uchumi miongoni mwa Watanzania wote.
Kwa upande wake msemaji wa familia ya Mwalimu Nyerere, Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Sinde Warioba alizungumza kwa uchache wakati wa kuanza rasmi kwa msafara wa waendesha baiskeli nyumbani kwa Mwalimu, Msasani jijini Dar es Salaam kwa kusema, “nimefurahi kuona tukio hili limeweza kukusanya nchi tofauti zikiwemo zote za Afrika ya Mashariki kitu ambacho kinaonyesha mshikamano wetu. Njiani mtakapopita mtaweza kujionea nchi yetu ya Tanzania kwa upana wake na kupitia shughuli mtakazozifanya njiani zitawanufaisha Watanzania. Ni matumaini yangu kuwa kupitia msafara wenu mtaweza kuhamasisha mabadiliko kwenye sekta ambazo mtaziangazia kama yalivyokuwa malengo ya Mwalimu. Bado sekta za elimu, mazingira na afya zina mchango mkubwa kwa manufaa ya umma na nimefurahi kuona mmejikita kwenye maeneo haya. Niwatakie kila la kheri muwapo njiani na bila shaka tutajumuika pamoja kuwapokea mtakapofika Butiama.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Vodacom Tanzania Foundation, Bi. Harriet Lwakatare, ambao ndio wadhamini wakuu wa msafara huo kwa 2023, ameongezea kuwa, “kama tulivyoeleza wakati wa uzinduzi wa ushirikiano wetu, tuna imani kubwa na Twende Butiama hususani kwa kile wanachokifanya katika kuenzi maisha na urithi wa Mwalimu. Elimu, afya, na mazingira ni vipaumbele vikubwa vya taasisi yetu na siku zote tupo mstari wa mbele kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha maeneo haya yanaboreshwa ili kuwanufaisha Watanzania sehemu tofauti nchini kote. Ningependa kutoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuunga mkono kampeni ya kuchangia dawati inayoendelea kupitia LIPA NAMBA 5483454, na kujumuika nasi katika shughuli za upandaji miti, na kushiriki kwenye kambi ya bure ya matibabu tutakayoiendesha.”

Kwa kumalizia Mwenyekiti wa Twende Butiama, Bw. Gabriel Landa amesema kuwa, “baada ya kuwatangazia Watanzania uwepo wa msafara wa Twende Butiama takribani wiki mbili zilizopita, hatimaye ile siku tuliyokuwa tunaisubiria kwa hamu imefika. Leo Oktoba mosi tukiwa hapa na washiriki takribani 200, tumeanza safari yetu kutokea nyumbani kwa Mwalimu, Msasani jijini Dar es Salaam na tunatarajia kufika Wilayani Butiama Oktoba 14. Tunawashukuru wadhamini wakuu wa mwaka huu, taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation, wadau, na Watanzania kwa ujumla wanaozidi kutuonyesha ushirikiano wao. Tukiwa njiani tutajihusisha na shughuli za kupanda miti, kuchangia madawati kwa shule za msingi za umma kwenye mikoa tofauti. Pia, tunawaomba watu wajitokeze kwa wingi kutuunga mkono njiani katika njia tutakazopita na kututia moyo.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: