Na Humphrey Shao, Michuzi TV.

Bohari ya Dawa nchini (MSD) imeeleza kuwa imefanikiwa kuimarisha hali ya upatikanaji na usambazaji wa dawa na huduma mbalimbali za kiafya nchini ikiwemo vifaa tiba kutokana na mabadiliko mbalimbali yanayoendelea kufanywa na Taasisi hiyo.

Hayo yamebainishwa Septemba 27, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji, mafanikio na mwelekeo wa Taasisi hiyo katika Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, kwa wahariri wa Vyombo vya habari kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).
Tukai amebainisha kuwa upatikanaji wa bidhaa za afya umeongezeka kutoka asilimia 51 mwezi Juni 2022 hadi kufikia asilimia 64 Juni 2023, ilihali upatikanaji wa Dawa umefikia asilimia 81 mwezi Juni 2023 kutoka asilimia 57 mwezi Juni 2022 huku akibainisha kuwa mapato ya Usambazaji yameongezeka hadi kufikia Tsh. Bilioni 52 sawa na asilimia 16.

“Fedha iliyopokelewa mwaka wa fedha 2022/23 ni Tsh. bilioni 190.3 ikilinganishwa na Tsh. bilioni 134.9 mwaka wa fedha 2021/22, sawa na asilimia 95, fedha hii imesaidia kuanzisha Kitengo Maalumu cha Usimamizi na Ufuatiliaji wa Mikataba, Ununuzi wa bidhaa za afya kutoka kwa wazalishaji wa ndani ambao umeongezeka kutoka Tshil bil 14.1 mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia shil bil 39.77.” amefafanua Mkurugenzi huyo.

Aidha Mkurugenzi huyo amesema kuwa MSD imeanzisha utaratibu wa kutokuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi zile ambazo zinakidhi mahitaji na viwango vya ubora kwa kuongeza ufanisi wa wazalishaji wa ndani, halikadhalika kuanzisha zabuni maalumu zinazohusu wazalishaji wa ndani hivyo kuongezea uwezo wa uzalishaji.
“MSD imefanikiwa kuongeza idadi ya mikataba ya muda mrefu kutoka mikataba 100 yenye bidhaa za afya 711 kwa mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia mikataba 233 yenye bidhaa 2,209 kwa mwaka wa fedha 2022/23,” amesema Mkurugenzi huyo.

Aidha katika usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini, MSD imeeleza kuwa imeimarisha mfumo huo kwa kusambaza bidhaa za afya mara 6 kwa mwaka ikiwa ni kila baada ya miezi miwili kwa mwaka wa fedha 2022/23 kinyume na ilivyokuwa hapo awali ambapo usambazaji ulifanyika kila badala ya mara 4 kwa mwaka (miezi mitatu) hivyo kupunguza muda wa vituo vya afya kusubiri bidhaa za afya.

“MSD imefanikiwa kununua matrela 16 yenye thamani ya Tsh. bilioni 2.6 ili kuongeza kasi ya usambazaji wa bidhaa za afya, ambapo kwa sasa usambazaji wa bidhaa za afya umeongezeka kwa asilimia 16 kutokana na kuongezeka kwa bajeti ya usambazaji kutoka Tsh. bilioni 320 kwa mwaka wa fedha 2021/22 hadi Tsh bilioni 373 kwa mwaka wa Fedha 2022/23, lakini pia MSD imekuwa inatumia mifumo shirikishi ya TEHAMA (PoD) ili kuhakikisha bidhaa za afya zinapokelewa kielekroniki katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa magari kwa kutumia mifumo,” Ameeleza Mkurugenzi huyo.
Aidha Tukai amesema katika kuhakikisha MSD inakidhi upatikanaji na usambazaji wa dawa kwa ufanisi zaidi na kwa kiwango kikubwa nchini, kwa sasa Taasisi hiyo inaendelea na uwekezaji wa shughuli mbalimbai ikiwemo ukamilisaji wa Ujenzi wa Kiwanda cha mipira ya mikono “gloves” kilichopo Idofi, Mkoani Njombe, Utekelezaji wa Mradi wa Ununuzi na Usambazaji wa vifaa vya huduma kwa wajawazito wanaopata uzazi pingamizi wakati wa kujifungua (CEmONC) ambao utatekelezwa kwa awamu tano huku ikitarajiwa kujengwa vituo 284 vya kutolea huduma vitavyopokea vifaa vya tiba.

Tukai amesema, “Katika mradi huo, Jumla ya vifaa vilivyopangwa kusambazwa ni 345, ambapo mpaka sasa vifaa vilivyosambazwa hadi kufikia Juni 2023 ni 299, ikiwa ni sawa na asilimia 87,” na kuongeza kuwa MSD imejipanga ili kuhakikisha kuwa inahusisha sekta binafsi kwa kutambua maeneo ya uwekezaji ya bidhaa za afya za kimkakati za vidonge (tablets), rangi mbili (capsules) na vimiminika

Lakini pia MSD inaendelea na kukamilisha taratibu za usajili na uendeshaji za kiwanda cha barakoa cha N95 kilichopo Keko ambapo uzalishaji wake utakidhi mahitaji ya barakoa nchini pamoja na uanzishaji wa Kampuni Tanzu “MSD Medipharma Manufacturing Company Ltd” itakayosimamia uzalishaji wa bidhaa za afya.

Kuimarisha uhifadhi wa bidhaa za afya kwa kujenga maghala ya kisasa mikoa ya Kagera, Dar es Salaam na Mwanza lakini pia kusimika na kuimarisha matumizi ya TEHAMA kwenye kazi zote za Taasisi pamoja na kuimarisha matumizi ya takwimu kwenye kazi zote.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: