Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habib Suluo.

................
Na Dotto Mwaibale, Singida

MKURUGENZI Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habib Suluo, ameihakikishia Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuwa mamlaka hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuboresha shughuli za usafirishaji nchini na kuwapima madereva ili waendeshe vyombo vya moto kwa usalama zaidi.

Suluo aliyasema hayo baada ya Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Miraji Mtaturu, kuipongeza LATRA kwa kusimamia mfumo utoaji wa tiketi kwa mtandao ambao umeanza kupunguza kero kwa abiria.

'' Tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa ukamilifu na kuufanyia kazi ushauri uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa lengo la kuboresha shughuli za usafirishaji ikiwemo kuendelea kuwatahini madereva ili kuhakikisha abiria wanasafiri kwa usalama,''. alisema Suluo wakati akiwasilisha taarifa ya mamlaka hiyo kwa wabunge wa kamati hiyo Agosti 25, 2023.

LATRA katika kuhakikisha inadhibiti mawakala wa mabasi wanaokwepa kukata tiketi kwa mfumo wa mtandao, LATRA Mkoa wa Singida juzi iliyatoza faini ya Sh. 250,000 kila basi kwa mabasi matano na kuvuna jumla ya Sh. 1, 250,000.

Mabasi yaliyotozwa faini hizo ni ya Kampuni ya Nyahunge mabasi manne na basi moja la kampuni ya Supafeo ambapo mabasi hayo yalikumbana na adhabu hiyo kutokana na kuwakatia abiria tiketi za zamani ambazo sio za kielektroniki zilizopigwa marufuku.

Hatua ya LATRA Mkoa wa Singida kuyatoza faini mabasi hayo ilikuja baada ya mmoja wa wasafiri waliokuwa ndani ya mabasi hayo kutoa taarifa kwa Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Singida, Layla Dafa kuwepo kwa abiria waliokatiwa tiketi ambazo sio za kielektroniki.

Baada ya Dafa kupewa taarifa hizo, alimtuma Afisa wake aitwaye Kilua Mbezi kuyafutilia mabasi hayo Stendi Kuu ya Mabasi Mkoa wa Singida ya Misuna na kubaini kosa hilo na kuyatoza faini.

Abiria waliokuwemo kwenye moja ya mabasi hayo walimpongeza Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Singida kwa kulifanyia kazi suala hilo kwa haraka na waliomba kuendelea na moto huo wa kazi hasa pale wanapopata taarifa kutoka kwa abiria na kuchukua hatua kwa haraka kama walivyofanya kwani mara nyingi katika maeneo mengine maafisa hao huwa hawafiki eneo la tukio jambo linalowakatisha tamaa na kuendelea kukithiri kwa vitendo hivyo.

Afisa wa LATRA Mkoa wa Singida Kilua Mbezi baada ya kuyatoza faini mabasi hayo alitoa elimu kwa abiria kuhusu umuhimu na faida ya kupatiwa tiketi za mtandao na kuwa kabla ya kupanda gari nilazima wapatiwe tiketi hizo na kama watawakatalia na kuwapa za zamani ambazo zimepigwa marufuku watoe taarifa kwa kupiga namba ya bure 0800110020.

Mbezi pia aliwakumbusha wafanyakazi wa mabasi hayo kuendelea kufuata sheria za usafirishaji ili kuepuka adhabu mara watakapobainika kutenda makosa na kuwa jambo hilo lipo ndani ya uwezo wao na kuwa wataendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa elimu hiyo.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Miraji Mtaturu akizungumzia baadhi ya faida za mfumo wa ukataji wa tiketi kimtandao (Kielektroniki) alisema ni pamoja na kupunguza mianya ya uvujaji wa mapato kwani abiria ana uhuru wa kukata tiketi basi analolitaka na mmiliki wa basi anaona idadi ya siti zilizokatwa tofauti na zamani na kuwa faida hizo zipo kwa wahusika wote, abiria, wafanyakazi wa mabasi hayo mmiliki na Serikali.

“Tunawapongeza sana LATRA sababu kupitia mfumo wa tiketi mtandao abiria anaweza kukata tiketi akiwa popote bila kulanguliwa na mawakala , lakini pia mfumo huu umerahisisha ukusanyaji wa mapato kwa wamiliki na Serikali sababu unaweza kuona idadi za tiketi moja kwa moja kupitia mfumo,’’ alisema Mtaturu.

Mara baada ya mfumo wa Tiketi Mtandao kuanza kufanya kazi rasmi Julai 1, 2022, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilifanya mkutano na wadau wa usafirishaji kutathmini utekelezaji wa mfumo huo na kujadili changamoto zinazojitokeza ili kuzifanyia kazi ikiwa ni pamoja na ukataji wa tiketi kimtandao.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Miraji Mtaturu akiipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kusimamia Mfumo wa Tiketi Mtandao kwani umepunguza kero kwa abiria wa usafiri wa ardhini nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habib Suluo. akizungumza katika kikao kazi na mmoja wa maafisa wa jeshi la Polisi kuhusu masuala ya usafirishaji.

Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Singida, Layla Dafa, akizungumza katika moja ya mikutano na wananchi, Iguguno wilayani Mkalama mkoani hapa kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na LATRA.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: