Wakati maelfu ya Watanzania kutoka kila pembe ya nchi wakiacha shughuli zao na kuelekea Lupaso kushuhudia ‘Wenye Nchi,’ Klabu ya Simba ikiukaribisha msimu mpya kwa tamasha lililofana, kikosi cha timu ya wafanyakazi wa Benki ya CRDB jana kiling’ara kwenye tamasha la Simba Day baada ya kuwanyamazisha wapinzani wao, Benki ya NMB kwa ushindi wa bao 1-0.

Kwenye tamasha hilo ambalo Simba iliendeleza utamaduni wake wa kuujaza uwanja kwa mashabiki wenye ari kubwa ya kuishangilia, walipata burudani murua kutoka kwa maofisa wa benki hizo mbili kubwa zaidi nchini walioziacha suti zao na kutupia bukta na fulana na kukiwasha mbele ya wapenda soka 60,000 walioujaza Uwanja wa Taifa almaarufu kama Uwanja wa Benjamini Mkapa au Lupaso jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kupata ushindi huo, Kapteni wa Timu ya Benki ya CRDB, Nicodemus Milinga amesema ilikuwa ni lazima washinde kwani walijiandaa vilivyo.

“Kujituma na kufuata maelekezo ya kocha. Wote tulikuwa na ari ya juu ya kuipigania brand (nembo) kama vile tunavyotoa huduma bora kwa wateja wetu kila siku, ndani na nje ya nchi,” amesema Milinga.

Twaha Beimbaya, kocha aliyejifunzia Uingereza na akaja akachukua kombe la U17 na JKT Tanzania mwaka 2021 halafu akaisaidia Pan Africa isishuke daraja la kwanza mwaka jana anayeinoa timu ya Benki ya CRDB, anasema uzoefu walioupata kwa kushiriki michuano ya Sikukuu ya Mei Mosi walikomenyana na vikosi vigumu vya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, umewaongezea kujiamini wachezaji wake.

“Tulipotoka huko, niliwaomba wachezaji kuhakikisha wanapata muda wa kufanya mazoezi ndio maana walikuwa vizuri kwenye pambano hili lililoshuhudiwa na mashabiki wengi zaidi nchini,” amesema Beimbaya.

Bao hilo pekee katika msimu huu wa 15 wa Simba Day, liliwekwa kimiani na mshambuliaji makini Abdallah Magohe baada ya makosa ya kipa wa Benki ya NMB kuanzisha mpira kimakosa hivyo kuwapa Benki ya CRDB ushindi ulioshangiliwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Abdulmajid Nsekela.

Kipindi cha kwanza cha mchezo huo uliokuwa burudani tamu kwenye tamasha hilo kutokana na soka la kitabuni lililoonyeshwa na timu zote huku washindi wakifunika, kilimalizika bila milango ya timu hizo kufunguliwa.

Kocha wa timu ya Benki ya NMB, nyota wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein almaarufu kama Mmachinga alikiri kuzidiwa na wapinzani wao waliotumia nafasi waliyoipata kushinda mchezo huo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: