Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware (wapili kulia) akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela leseni ya kuanzisha kampuni tanzu ya huduma za bima CRDB Insurance Company Ltd katika hafla iliyofanyika leo katika hoteli ya Gran Melia jijini Arusha. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Insurance Company, Gerald Kasato (wakwanza kulia), na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance Company, Wilson Mnzava.
---
Arusha 17 Mei 2023 - Katika kutanua huduma za bima nchini, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeipa Benki ya CRDB leseni kuanzisha kampuni tanzu ya kampuni ya bima ijulikanayo kama CRDB Insurance Company (CIC) Ltd hivyo kuwa benki ya kwanza nchini kumiliki kampuni kamili ya bima.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi leseni hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Gran Melia jijini Arusha, Dkt Baghayo Saqware, ameipongeza Benki ya CRDB kwa kukua katika utoaji wa huduma za bima kutoka kuwa wakala mpaka kampuni kamili ya bima.
“CRDB Insurance ni mtoto mpya kwenye soko la bima na mtoto mwingine kwa Benki ya CRDB kwenye soko la fedha nchini. Inafurahisha kuona mnakua kutoka hatua moja kwenda nyingine. Naamini ndani ya miaka mitano ijayo mtaenda kwenye hatua nyingine kubwa zaidi ya hii. Kuna fursa kubwa kwenu kukua katika soko letu,” amesema Dkt. Saqware.
Dkt. Saqware alisema kwa uzoefu ambao Benki ya CRDB inao katika sekta ya bima, TIRA ina imani CRDB Insurance Company (CIC) Ltd itakwenda kusaidia utekelezaji wa lengo la Serikali la kuchochea ujumuishi wa wananchi kwenye huduma za bima ili Watanzania wanaotumia bidhaa zake wawe walau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 kutoka asilimia 18 ya sasa.
“Katika kuchochea ujumuishi wa kibima Serikali imepitisha sheria ya kufanya baadhi ya bima kuwa za lazima ikiwamo bima ya majengo, makandarasi, afya, na za vyombo vya usafiri. Mkiweza kuja na mkakati madhubuti wa kuchangamkia vizuri maeneo haya na kuhudumia kwa walau asilimia 30 niwahakakikishie ndani ya kipindi kifupi mtatoka kuwa kampuni changa na kuwa moja ya kampuni kubwa za bima nchini,” amesema Dkt Saqware.
Akipokea leseni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema ni furaha kubwa kwao kupata leseni ya huduma za bima za jumla yaani ‘general insurance’ ukiwa ni muda mfupi tangu walipopata leseni ya kutoa huduma za benki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Benki ya CRDB inayo historia kubwa ya kufanya biashara ya bima kwani takriban miaka 15 iliyopita imekuwa ikiifanya kwa namna tofauti ikianza kama wakala na sasa ni kampuni kamili ya bima. Mafanikio haya yanadhihirisha mazingira rafiki ya kufanya biashara nchini,” amesema Nsekela.
Nsekela amesema kampuni ya CRDB Insurance Company itajikita katika ubunifu wa bidhaa na huduma za bima za jumla “general insurance” kwa kuzingatia viwango vilivyo bora na kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi walio wengi ili kuchcohea maendeleo ya uchumi wa nchi.
“Malengo yetu ni kuwa kiongozi katika sekta ya bima nchini kama ilivyo kwa Benki yetu na kampuni zetu tanzu nyengine. Lakini ili kuwa kiongozi ni lazima tuweze kutoa huduma zilizo bora na za mfano katika soko, lazima tuweze kuwekeza katika miundombinu ya usambazaji na uuzaji wa bima ikiwamo kuwatumia mawakala, madalali, banc assurance, na majukwaa ya kidijiti kuuza bima. Naomba nikuhakikishie Kamishna tumejipanga kutekeleza hayo yote,” amesema Nsekela.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance Company Ltd, Wilson Mnzava amesema wamejipanga kikamilifu kuanza kutoa huduma za bima kwa wananchi kuanzia bima zote za jumla huku akielezea kuwa tayari kampuni hiyo imeshaanza mchakato wa kuleta huduma bunifu za bima katika sekta za kimakati nchini ikiwamo sekta ya kilimo.
“Napenda kuwakaribisha Watanzania wote binafsi, taasisi, na kampuni kupata huduma katika kampuni yao ya CRDB Insurance Company Ltd. Niwahakikishie wananchi kwamba CRDB Insurance Company Ltd ndio chaguo sahihi kwao. Tumejiandaa kikamilifu kuwahudumia. Nikuahidi Kamishna kuwa kampuni yetu itashirikiana kwa karibu na TIRA kuboresha huduma na kuyafikia matarajio ya sekta ya bima kwa ujumla,” amesema Mnzava.
Taarifa za TIRA zinaonyesha mpaka Desemba 2022, kulikuwa na kampuni 32 za bima nchini hivyo CRDB Insurance Compaany Ltd inakuwa kampuni ya 33. Katika kipindi hicho, pia kulikuwa na mawakala wa bima 1,500, benki 32 zinazotoa huduma za bima na kampuni tano zinazotoa huduma za bima kidijitali.
Kwa sasa sekta ndogo ya bima inachangia asilimia 1.68 kwenye pato la taifa, malengo yaliyopo ni kufikisha asilimia tatu hadi mwaka 2030 na dalili za kufanikisha hilo zinaonekana kwani mwaka 2022 tozo za bima zilizolipwa (premiums) zilikuwa na thamani ya TZS 1.154 trilioni kutoka TZS 913 bilioni mwaka 2021.
Toa Maoni Yako:
0 comments: