Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Kiongozi wa Mabalozi nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed katika sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya Italia, jana jioni Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake katika sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya Italia, jana jioni Jijini Dar es Salaam
Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi akiwasilisha hotuba yake katika sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya Italia, jana jioni Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akikata keki katika sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya Italia, jana jioni Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi wakishangilia baada ya kukata keki katika sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya Italia, jana jioni Jijini Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu, Dar

Tanzania na Italia zimeahidi kushirikiana kukuza na kuendeleza sekta ya biashara ya uwekezaji kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Akihutubia sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya Italia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) alisema Tanzania imeboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kuwasihi wafanyabiashara wa Italia kuja kuwekeza nchini kwa kuwa ni salama zaidi.

“Natumia fursa hii kuwahakikishia ushirikiano wetu wa kukuza na kuendeleza biashara na uwekezaji nchini, Serikali imechukua jitihada mbalimbali za kuwavutia wawekezaji kuwekeza hapa nchini ikiwemo kuondoa vikwazo vya biashara,” alisema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula aliongeza kuwa, Tanzania na Italia zimekuwa na utamaduni wa kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kupitia majukwaa mbalimbali ya biashara na matokeo chanya ya majukwaa hayo yameanza kuonekana ambapo Disemba, 2021 kupitia kongamano la biashara na uwekezaji lililofanyika Italia, kampuni ya Kiitaliano ‘Suness Limited’ inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ilisaini makubaliano na Shirika la Taifa la madini (Stamico) kwa ajili ya kuendeleza mradi wa shaba inayopatikana Kilimanjaro.

“Ni Imani yangu kuwa kupitia kongamano la biashara na uwekezaji litakalofanyika mwezi Septemba 2022 Jijini Dar es Salaam na Zanzibar litatoa fursa nyingi zaidi kwa pande zote mbili kuchangamkia fursa zinazopatikana kwenye sekta za kilimo, viwanda, miundombinu, elimu, utalii na uchumi wa buluu,” alisema Balozi Mulamula

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula aliishukuru Serikali ya Italia kwa ushirikiano imara wa kuchangia maendeleo ya Tanzania ambapo wiki ijayo Tanzania na Italia zitasaini makubaliano ya mkopo wa masharti nafuu wa Euro milioni 20 kwa ajili ya kuboresha elimu ya ufundi katika mikoa ya Mbeya, Arusha, mwanza, Songwe, Zanzibar na Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi ameipongeza Tanzania kwa jitihada kubwa za kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara nchini.

“Kwa kweli tunafurahishwa sana na namna mazingira ya biashara yanavyoboreshwa hapa Tanzania, kwa kweli tutaendelea kuwashawishi wafanyabiashara wetu waje kuwekeza hapa kwani ni sehemu salama uya kuwekeza,” alisema Balozi Lombardi

Aliongeza kuwa kitendo cha Tanzania kuviondoa vikwazo vya biashara kimeongeza imani kubwa kwa wafanyabiashara na wawekezaji wengi duniani kuiona Tanzania ni salama. Aidha, Balozi Lombard alimpongeza Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuimarisha Diplomasia ya Uchumi na mataifa mengine duniani.

“Napenda kuwahakikishia kuwa Italia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuimarisha uhusiano uliopo baina yetu kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” aliongeza Balozi Lombardi.

Tanzania na Italia zimekuwa zikishirikiana katika Nyanja za kilimo, afya, elimu, maji, nishati, utalii na maendeleo ya sekta binafsi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: