Bw. Sosthenes Kewe kutoka FSDT (wa pili kushoto) akifafanua jambo wakati wa kongamano hilo ambalo limeshirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya ubunifu na wabunifu. Wengine katika picha hiyo ni viongozi wa taasisi , kampuni na mashirika mbalimbali wakisikiliza majadiliano kabla ya kutoa maoni yao.
Sehemu ya washiriki wakiwa makini kufuatilia mijadala, maoni na michango kuhusu bunifu na wabunifu nchini hasa katika kuangalia mbinu mbalimbali ambazo zitasaidia kuendeleza wabunifu na kada nyingine za aina hiyo.
Mkurugenzi Mkuu Kampuni ya Phema Agri, Bi. Daniela Kwayu (wa tatu toka kulia) akitoa mchango kuhusu ambavyo wamekuwa wakisaidia wakulima katika masuala mbalimbali yanayohusu kilimo na teknolojia. Wengine ni Ofisa kutoka COSTECH Bi. Promise Mwakale (wa pili toka kushoto). Wa kwanza kushoto ni Bw. Sosthenes Kewe kutoka FSDT na Bw. Salim Awadh.
Meneja Mratibu wa Miradi kutoka Funguo Bw. Joseph E.M akizungumza wakati wa kongamano hilo ambapo ameeleza kwa kina kuhusu ushiriki wao katika kuendeleza sekta ya ubunifu.
Sehemu ya wadau wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza kwa kipindi cha kwanza cha Kongamano maalum la majadiliano kuhusu sekta ya ubunifu na wabunifu. Kongamano hilo limefunguliwa leo Mei 10, 2022 jijini Dar es Salaam na limeandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa kushirkiana na COSTECH pamoja na UNDP kupitia Programu yake ya Ubunifu –Funguo na mdhamini Mkuu ni Kampuni ya Simu ya Voda-Tanzania.
Na Cathbert Kajuna - Kajunason, Dar es Salaam
Wadau wa masuala ya Ubunifu nchini Tanzania wameomba serikali kusimamia vyema masuala ya Ubunifu ila yaweze kuleta tija katika jamii zao.
Hayo yamesemwa katika Kongamano la ubunifu ambalo limeandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) linaloendelea katika wiki ya Ubunifu iliyozinduliwa leo Mei 10, 2022 jijini Dar es Salaam na wadau hao wamepata nafasi ya kujadili kwa kina masuala yanayohusu ubunifu na hatua wanazochukua kuendeleza sekta ya ubunifu ili kuwa na tija kwa Watanzania.
Mkurugenzi wa Tafiti, Sera na Mipango katika Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Bw. Alfred Mkombo akizungumza mbele ya wabunifu na wadau hao amesema kazi yao ni kusimamia masoko ya mitaji ili biashara zinazohitaji mitaji zinapata kupitia utaratibu uliopo.
“Leo tumekuwa na kongamano hili kuangalia ubunifu katika maeneo ya biashara zinazoanza na biashara za kati kwamba namna gani hizi biashara zinapata mitaji kupitia masoko ya mitaji.
“Sisi kama Mamlaka ya Masoko na mitaji tunasaidia ubunifu katika masoko ya mitaji. Mojawapo ya jukumu letu ni kuendeleza masoko ya mitaji na ili kuendeleza lazima usimamie ubunifu, biashara ya ubunifu na ubunifu katika bidhaa na huduma zinazohitajika kwa wananchi.
“Kwa hiyo sisi tunawachagiza wananchi hasa vijana wawe wabunifu zaidi. Sasa hivi tuna mpango ambao tunafanya kwa ushirikiano na UNDP katika kutengeneza miongozo ya kusimamia mipango ya mitaji shirikishi.Tunaposema mitaji shirikishi ni utaratibu wa kupata fedha kwa ajili ya kuendeleza mradi fulani unapata fedha,”amesema Bw. Mkombo.
Amefafanua kuwa mtu anachanga fedha kidogo kidogo kama inavyofanyika msibani au kwenye makanisa lakini ile fedha sasa wanaichukua na wanaipeleka kwenye uzalishaji.
“Ukusanyaji huu unakuwa tofauti kidogo kwasababu unakusanywa kupitia mitandao au majukwaa ya mitandao ya kieletroniki na hii mitandao ni lazima iwe imesajiliwa, kwa hiyo tunafanya huo mpango japo kwasasa tunaandaa miongozo kwa ajili ya uendeshaji.”
Kwa upande wake Ofisa kutoka COSTECH Bi. Promise Mwakale amesema wamekuwa wakitoa ruzuku kwa ajili ya wabunifu na wanatoa ruzuku kuanzia kwenye mawazo na kuwakuza.“Kwa hiyo Kongamano hili ni muhimu kwetu kwani limejumuisha wadau wengine katika kufungua masoko na kuongeza mitaji kwa ajili ya wabunifu”amesema Mwakale.
Nae Mtalaamu wa Fedha kutoka UNCDF Bw. Paul Damocha amesema wao mbali ya kuwa moja ya wadhamini wa Wiki ya Ubunifu kwa nyakati tofauti wamekuwa wakishiriki katika kukuza na kuendeleza ubunifu kwa njia tofauti kwa kushirikiana na Serikali, COSETCH na wadau wengine.
Ameongeza kuwa wamekuwa wakisaidia katika sekta ya fedha, sera na kutengeneza miongozo pamoja na kuelekeza idara za Serikali katika kutengeneza mazingira wezeshi kwa wabunifu na kuwapatia leseni.
“Kumekuwa na jitihada kubwa za kitalaam za kusaidia wajasiriamali kuanzisha biashara zao, mambo ya teknolojia na biashara. Kuhusu ubunifu tunaona haja ya kushirikisha washika dau wengi yakiwemo mashirikia makubwa.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Kampuni ya Phema Agri, Bi. Daniela Kwayu amesema wao wamejikita katika kutumia teknolojia kuwasaidia wakulima pamoja na kuwawezesha katika pembejeo.
Kuhusu ushiriki wao kwenye Kongamano la Ubunifu amesema wao ni miongoni mwa kampuni ambazo zimepata msaada mkubwa kutoka CMSA, hivyo wameshiriki ili kutoa shuhuda jinsi walivyofanikiwa na kusaidia wakulima wengi nchini.
Wiki ya Ubunifu Tanzania ambayo kilele chake kitafanyika Dodoma Mei 16, 2022 inaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikishirikiana na COSTECH na UNDP kupitia programu ya Ubunifu - FUNGUO huku mdhamini mkuu akiwa Vodacom Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments: