Na Grace Semfuko, MAELEZO, Dar
Oktoba 7, 2021.
Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya kufuatilia mwenendo wa maafa na kutoa tahadhari ya mapema kwa umma, ili kupunguza madhara yatokanayo na hali hiyo pamoja na kujiandaa na kukabiliana nayo.
Ili kuhakikisha tahadhari za maafa yanayotokana na hali mbaya ya hewa zinatolewa kwa uhakika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaandaa jukwaa la mfumo wa kidigitaji kwa ajili ya uchambuzi wa hali hewa, ili kubaini madhara ya mafuriko na ukame na kuchukua hatua stahiki za usimamizi wa maafa kwa wakati.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa, itakayofanyika Oktoba 9 hadi 13 kwenye Mikoa ya Dodoma na Geita, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu Bw. Tixon Nzunda, amesema Serikali itaendelea kuboresha sera, sheria na kuandaa mikakati kwa lengo la kuimarisha mfumo wa uratibu na usimamizi wa maafa nchini.
"Maonyesho ya wazi yatafanyika Viwanja vya Mazania, Wilayani Chato Mkoani Geita Oktoba 09 hadi 13, 2021 na Viwanja vya Nyerere Square, Dodoma Oktoba 11 hadi 13, 2021 na kwa maeneo yote hayo kilele itakuwa Oktoba 13, shughuli zitakazotekelezwa katika maadhimisho haya ni utoaji wa elimu kwa umma ili jamii itambue aina za majanga na vyanzo vyake, madhara ya maafa, kupunguza athari zake na namna ya kujiandaa kukabiliana nayo, nawaomba wananchi wajitokeze ili kupata elimu ya kukabiliana na maafa” alisema Bw. Nzunda.
Bw. Nzunda pia alibainisha kuwa, Serikali imeandaa mipango ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika halmashauri 20 zilizoonekana kuwa katika hatari kubwa ya kuathirika na maafa kwa kuzingatia wajibu wa sekta katika usimamizi wa maafa na huduma za kibinadamu.
"Halmashauri zilizoandaliwa mipango ya dharura ni Chamwino, Kondoa, Mpwapwa, Shinyanga Vijijini, Kishapu, Bariadi, Maswa, Meatu, Mwanga, Same, Kilosa, Mvomero, Kilombero, Mtwara Manispaa, Halmashauri ya Mtwara, Masasi, Bukoba Manispaa, Bukoba halmashauri, Meru, na Liwale, Maandalizi ya mipango yalienda sambamba na kufanyika tathmini ya majanga makuu yaliyopo, kupitia programu mbalimbali” alisema Bw. Nzunda.
Aidha alibainisha kuwa Serikali kwa kuzingatia wajibu wa sekta katika usimamizi wa maafa na huduma za kibinadamu, imeandaa Mipango na Miongozo ya Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa ya Sekta mbalimbali.
Mwisho.
Toa Maoni Yako:
0 comments: