Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akitazama mtambo uliobuniwa na TGDC wenye uwezo wa kukusanya taarifa za kisayansi za utafiti wa nishati ya jotoardhi na kuzituma kwa njia ya simu bila ya kuhitaji mtaalam kuwa eneo la utafiti.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akiwakabidhi wanakijiji wa eneo Majimoto (katikati) kuku walio totolewa na kukuzwa kutokana na nishati ya jotoardhi, kushoto ni Meneja Mkuu TGDC Mhandisi Kato Kabaka.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akigusa maji ya moto katika mojawapo wa chemchem ya majimoto ambacho ni chanzo cha nishati ya jotoardhi katika enelo la Majimoto mkoani Songwe, katikati ni Meneja Mkuu TGDC Mhandisi Kato Kabaka na Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Biashara TGDC Mhandisi Shakiru Kajugus (kushoto).
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akipatiwa maelezo ya mradi wa uendelezaji nishati ya jotoardhi katika eneo la Majimoto lililoko mkoani Songwe, anayetoa maelezo ni Meneja Mkuu TGDC Mhandisi Kato Kabaka (aliyeshika kijiti).

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ameeleza kuwa mikoa ya Mbeya na Songwe inavyanzo vya nishati ya jotoardhi vyenye uwezo wa kuzalisha megawati 165 za umeme nishati ya jotoardhi.

Amesema hayo alipotembelea eneo la majimoto lililoko wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.

Ameeleza kuwa miradi ya kipaumbele ya Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) ya Ngozi (Mbeya), Songwe (Songwe), Kiejo Mbaka (Mbeya), Natron (Arusha) na Luhoi (Pwani) yote inao uwezo wa kuzalisha megawati 200.

“Tunaanza na megawati 200 mojawapo ikiwa ni kutoka katika mradi huu wa jotoardhi Songwe, huku eneo hili peke yake likiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 5 hadi 38,” alisema Dkt. Kalemani.

Aliendelea kueleza kuwa ili kufikia lengo la megawati 200 itahusisha miradi mingine ya jotoardhi ya kipaumbele iliyoko chini ya TGDC.

“Tanzania licha ya kuwa na jumla ya megawati 1602 kwa sasa lakini bado hatuna hata megawati moja ya jotoardhi, ndio tunataka sasa tuharakishe,” aliongezea Dkt Kalemani.

Alielekeza kuharakishwa kwa shughuli zinazo endelea za uendelezaji nishati hiyo ili ndani ya miaka mitatu ijayo nchi iianze kunufaika na umeme wa nishati wa jotoardhi.

“Ningependa kuipongeza serikali yetu kwa kutupatia shilingi bilioni 20 mwaka jana ili kuhakikisha miradi hii inayotekelezwa,” alifafanua Dkt. Kalemani.

Aliongeza kuwa shughuli zilizofanyika mpaka sasa zimegharimu shilingi bilioni 1.029 na kwamba bado kuna fedha za kutosha kuendeleza shughuli za uendelezaji nishati ya jotoardhi na hukakikisha umeme wa jotoardhi unapatikana.

Aliendelea kueleza kuwa wakati shughuli za uendelezaji wa nishati ya jotoardhi katika kuzalisha umeme zinaendelea na tayari TGDC imejiongoza kwa kutengeneza fursa kwa kutumia nishati ya jotoardhi kutotolesha vifaranga, kufugia samaki, ushughuli za utalii, kukaushia mazao na shughuli nyingine.

“Niwapongeze sana TGDC …unapokuwa na manufaa makubwa ya kutumia nishati ya jotoardhi kuzalisha umeme ukawa na manufaa mengine yanayo ambatana hayo ambayo tumeyataja ni jambo zuri,” alisema Waziri Nishati.

Alifafanua kuwa iliuweze kuzalisha umeme wa nishati ya jotoardhi kunahitajika nyuzi joto 100 hadi nyuzi joto 140, lakini joto linalopatikana kwa sasa ni nyuzi joto 70 mpaka 80 ambalo ndilo linalofaa kwa matumizi mengine ya nishati hiyo.

Alisisitiza kuwa shughuli za matumizi mengine ya nishati ya jotoardhi ni vyema kwa TGDC kuwashirikisha wananchi iliwaweze kunufaika na fursa ya uwepo wa nishati ya jotoardhi katika maeneo yao. 

Kwa upande wake, Meneja Mkuu TGDC, Mhandisi Kato Kabaka alieleza kuwa licha ya TGDC kuendelea na uendelezaji wa nishati ya jotoardhi katika uzalishaji wa umeme kuna teknolojia ambazo zimebuniwa na TGDC zikiwa na lengo la kuchangia katika shughuli za kiuchumi nchini.

“Mpaka sasa tumebuni teknolojia ya utotoleshaji vifaranga kwa kutumia nishati ya jotoardhi, kifaa cha kudhibiti joto la maji moto na kifaa cha kukusanya taarifa za utafiti wa nishati ya jotoardhi,” alieleza Mhandisi Kabaka.

Aliongeza kuwa shughuli za utafiti wa kina wa nishati wa jotoardhi katika miradi ya kipaumbele ya kuzalisha umeme zinaendelea na kwa sasa TGDC imefikia hatua ya uchorongaji visima vya jotoardhi ili kuhakiki kiwango cha hifadhi halisi ya jotoardhi iliyoko chini ya ardhi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: