Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiongea na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kudhibiti ugonjwa wa homa ya Nguruwe kwenye Mkutano uliofanyika jijini Dodoma juzi.
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga (kushoto) akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu ugonjwa wa homa ya Nguruwe katika Mkutano uliofanyika jijini Dodoma juzi. Kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki.

Na Mbaraka Kambona, 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha ugonjwa wa homa ya Nguruwe ulioikumba Mikoa ya Kanda ya Ziwa hivi karibuni unadhibitiwa, huku akisema kuwa tangu ugonjwa huo uanze mpaka sasa umeshasababisha vifo vya Nguruwe 1500 wenye thamani ya shilingi milioni 375. 

Ndaki aliyasema hayo juzi jijini Dodoma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuudhibiti ugonjwa huo uliokumba Mikoa ya Kanda ya Ziwa. 

Alisema kuwa vifo hivyo vimesababisha hasara ya moja kwa moja kwa wafugaji kwa sababu kipato hicho kilichopotea ilikuwa wakipate wafugaji huku akiwataka wafugaji hao kuwa watulivu na kufuata maelekezo ya serikali ili ugonjwa huo uweze kudhibitiwa kwa haraka. 

Aliongeza kuwa ugonjwa huo unaosababishwa na virusi unahama kutoka kwa nguruwe pori na Ngiri na unasambaa kupitia njia ya Maji, Damu au Kinyesi. 

Ndaki alisema kuwa Halmashauri zilizoathirika mpaka sasa ni Mbogwe, Kyerwa, Geita, Sengerema, Kahama na Misungwi na alibainisha kuwa serikali imeshachukua hatua kadhaa za kudhibiti ugonjwa huo. 

Alisema kuwa mpaka sasa serikali imeshachukua hatua mbalimbali za kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa ikiwemo kuweka karantini za mifugo hiyo ili kudhibiti ugonjwa huo usisambae zaidi. 

“Tumeongeza Wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Wataalamu kutoka Chuo cha Sokoine (SUA) na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) kwenda kuungana na wataalamu wa Halmashauri ili kuongeza nguvu ya kudhibiti ugonjwa huo,” alisema Ndaki. 

Ndaki alisisitiza kuwa ugonjwa huo hauna chanjo wala tiba huku akiwahimiza wananchi kuhakikisha wanazingatia maelekezo wanayopewa na wataalamu ikiwemo kupulizia dawa za kuua wadudu Kupe katika mabanda ili kuzuia ugonjwa huo usisambae zaidi. 

“Niwaombe wananchi waache kula nyama ya Nguruwe, hatua hizi tunazochukua lengo lake ni kudhibiti ugonjwa usiendelee kuleta madhara zaidi katika maeneo mengine,”alisema Ndaki. 

Aidha, Ndaki amewataka Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi katika maeneo yaliyoathirika kuhakikikisha wanasimamia kikamilifu karantini zilizowekwa na wataalamu ili ugonjwa huo kuzuiwa kusambaa katika maeneo mengine huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano ili hatua hizo zinazochukuliwa na serikali ziweze kuzaa matunda. 

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga alisema kuwa ili ugonjwa huo usisambae zaidi ni muhimu wafugaji kuhakikisha kuwa mifugo yao inakuwa katika mabanda wakati wote na kuacha kusafirisha mifugo na mazao yake kutoka sehemu moja kwenda nyingine kabla ya kupimwa na Daktari.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: