MBUNGE wa Viti Maalumu anaewakilisha Kundi la Asasi za Kiraia (NGOs) CCM Neema Lugangira akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi kati ya Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto na Mashirika yasiyo ya Kiserikali
MBUNGE wa Viti Maalumu anaewakilisha Kundi la Asasi za Kiraia (NGOs) CCM Neema Lugangira akizungumza wakati wa kikao kazi kati ya Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto na Mashirika yasiyo ya Kiserikali

MBUNGE wa Viti Maalumu anaewakilisha Kundi la Asasi za Kiraia (NGOs) CCM Neema Lugangira amesema kwamba Sekta ya Azaki bado inahitaji kujengewa uwezo haswa NGOs ndogo ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa tija kubwa .

Hayo aliyasema wakati alipokutana na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali(NGOS) kwa upande wa Tanzania bara kwenye Kikao Kazi cha Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto na Mashirika hayo.

Kikao hicho ambacho amekutana na Sekta ya Azaki (NGOs) kwa mara ya kwanza, Mbunge Neema alisema ushirikiano kati ya Bunge, NGOs na Serikali ni muhimu kwakuwa wote ni wadau wa maendeleo na kazi yao ni kuhudumia wananchi.

Mbunge Neema Lugangira alipendekeza mambo mawili; kwanza NGOs kubwa za Kitaifa ziwe na utayari wa kufanya kazi na NGOs ndogo na pili NGOs za Kimataifa na Wadau wa Maendeleo waelekezwe juu ya umuhimu wa kuhakikisha sehemu ya fursa walizonazo zinakwenda kwa NGOs ndogo.

Alisema kwamba hiyo yatasaidia kuwajengea uwezo NGOs ndogo na hatimae kujenga mazingira wezeshi ya NGOs ndogo ili nazo zikue na kutimiza malengo yake vizuri. 

Mbunge Lugangira huyo alisema ili NGOs ziweze kuthaminika na kutambulika kwa kazi kubwa inayofanyika katika kuleta maendeleo kwa jamii ni lazima NGOs zifanye kazi kwa uwazi na uwajibikaji.

“ Kwani kwa kufanya hivi pamoja na mambo mengine, itaiongezea nguvu hoja zinazowasilishwa na Sekta hii muhimu ya NGOs kwenda Serikalini na Bungeni” Alisema Mbunge huyo.

Hata hivyo Mbunge Neema alitoa ushauri kwa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo Ya Kiserikali "NACONGO" ianze kutekeleza muundo wake wa kuwa na uwakilishi wa NGOs ngazi zote kuanzia Wilaya, Mkoa hadi Taifa kupitia Mabaraza ya Wilaya, Mikoa hadi Taifa.

“Hii itasaidia kuratibu mipango ya Serikali na NGOs kwenda sambamba na pia hili litanisaidia sana mimi kama Mbunge wa Viti Maalumu ninaewakilisha kundi la NGOs Bungeni maana ninahitaji kukutana na NGOs Wilayani, Mikoani na Taifani kupitia mfumo rasmi kama huu wa NACONGO hivyo ni muhimu sana Mabaraza haya ngazi zote yawepo na yafanye kazi” Alisema Mbunge huyo.

Mbunge huyo aliwahakikishia Wadau wa Sekta ya NGOs kuwa atakuwa Mwakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali/Asasi za Kiraia (NGOs) Bungeni ikiwemo kuwa tayari kushirikiana nao kuimarisha Sekta hiyo ya Azaki.

“Lakini pia niliwasilisha ombi langu la kushirikiana kwa karibu na Foundation for Civil Society kwa lengo la kufanyia kazi haya niliyowasilisha na mengine ambayo tutayajadili pindi tutakapokutana” Alisisitiza

Katika hatua nyengine Mbunge huyo aliwashukuru Wakurugenzi Wanawake 7 wa NGOs kutoka Jukwaa la Wakurugenzi Wanawake wa Azaki "CSO Women Directors Forum" ambao walikubali kutenga muda wao, kupitia na kuboresha maelezo yangu hadi kufanya zoezi la kuomba kura mbele yao ili kuhakikisha nitakuwa ndani ya muda.

Wakurugenzi hao ni Anna Kulaya, Jane Magigita, Dr. Astronaut Bagile, Christina Kamili, Geline Fuko, Utti Mwangamba na Irene Fugara.

“Kwa hakika huu ulikuwa Mkutano muhimu sana kwangu kushiriki na namshukuru sana Mhe Spika, Mhe Job Ndugai (Mb.) kwa kunipa ruhusa ya kutoka Bungeni na kushiriki Mkutano huu” Alisema Mbunge huyo

Aidha pia aliwashukuru Mhe Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, Mhe Naibu Waziri, Mhe Dkt. Mollel na Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Dkt. Jingu kwa ushirikiano wa mkubwa na kwa utambuzi wa nafasi yangu kama kiungo muhimu kati ya NGOs, Serikali, na Bunge.

"Sasa kazi iendelee na tuachane na tofauti ya itikadi zetu za kisiasa, tufanye kazi na mnitumie kama daraja kati yenu NGOs, Bunge na Serikali", alihitimisha Mbunge Lugangira
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: