Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza (kulia) akiwasilisha taarifa ya mpango wa usimamizi wa matumizi ya ardhi kimkoa na hatua za utekelezaji wake wakati Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alipofanya ziara ya kikazi kutembelea mkoa huo.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, anayesimamia Halmashauri za Singida Manispaa na Singida Vijijini, Mhandisi Paskas Muragiri akizungumzia mambo kadhaa yanayohusu maboresho kwenye sekta ya ardhi mbele ya Waziri Lukuvi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikagua mafaili na nyaraka zote zilizohifadhiwa ndani yake kwenye Masijala ya Ardhi Singida Vijijini alipofanya ziara kwenye eneo hilo, sanjari na kutoa maelekezo ya namna bora ya utunzaji wa kumbukumbu hizo kwa faida ya wananchi.
Waziri Lukuvi akitoa maelekezo juu ya maboresho kadhaa yanayopaswa kufanywa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, alipofanya ziara kwenye ofisi za ardhi ndani ya halmashauri hiyo. Kushoto ni Afisa Ardhi na Kaimu Mkuu wa Idara hiyo, Ambroce Ngonyani
Waziri Lukuvi akitoa maelekezo juu ya maboresho kadhaa yanayopaswa kufanywa ndani ya Manispaa ya Singida, alipofanya ziara kwenye ofisi za ardhi ndani ya Manispaa hiyo. Kulia ni Afisa Ardhi Mteule, Christian Kasambala.
Ziara ikiendelea.
Ziara ikiendelea.
Waziri Lukuvi akiwa kwenye ziara ya kukagua mashamba makubwa ya mradi wa Kilimo cha Pamoja cha Korosho ‘Block Farming’ yaliyopo eneo la Masigati Wilaya ya Manyoni. Kupitia ziara hiyo aliagiza wakulima wote kwenye maeneo hayo wapatiwe hati kwa ustawi zaidi wa maisha yao.
Ziara kwenye mashamba hayo ikiendelea.
Baadhi ya Watendaji Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Singida wakiwa na Waziri Lukuvi (hayupo pichani) kwenye ziara hiyo. Kutoka kushoto ni Naibu Kamishna wa wa ofisi hiyo Shamim Hoza, Msajili wa Hati Msaidizi Jamila Awadhi, Mpima Ardhi Mkoa Sesaria Lusingu na Afisa Mthamini Angelina Bauleni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Manyoni, Charles Fussi (kulia) akizungumza na Waziri Lukuvi kwenye ziara hiyo eneo la masigati, Manyoni.
Ziara ikiendelea.
Ziara ikiendelea.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameagiza Wakurugenzi nchini kuanza mara moja kuwapa wajibu Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji kufanya kazi ya kuratibu na kusimamia masuala yote yanayohusu shughuli za uendelezaji ardhi kwenye maeneo yao-isipokuwa kugawa na kuuza, ili kupunguza changamoto ya migogoro na kurahisisha ukusanyaji wa kodi na taarifa.
Lukuvi aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani hapa juzi, alipotembelea ofisi zote za ardhi kwenye Halmashauri za wilaya Singida Vijijini, Singida Manispaa, Ikungi na Manyoni.
“Nataka Wakurugenzi wote muwape wajibu kwa maandishi Maafisa Watendaji wote wa Mitaa na Vijiji kufanya kazi kama ‘Land Administrators’ kwenye maeneo yao. Na lazima tushirikiane nao kwa karibu kama jicho letu kule chini, fanyeni haraka jitihada ya kuwakutanisha pamoja na kuwapa uelewa kujua mambo gani ya kwenda kusimamia, hii itasaidia sana katika usimamizi wa pamoja wa ardhi,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“Nataka ieleweke huyu Mtendaji wa Mtaa sio jukumu lake kumilikisha wala kugawa ardhi, sababu hilo ni jukumu la kamati ya wilaya ya Manispaa. Yeye atahusika tu katika usimamizi wa kila kitakachofanyika na kwa kufanya hivyo tutapokea taarifa nyingi na kwa haraka sana juu ya uendelezaji holela, ukwepaji kodi na uvunjifu wa sheria. Tukiheshimu na kufuata utaratibu huu tutapiga hatua kubwa kwenye makusanyo.
Aidha, aliwataka wananchi wote kutofanya chochote kinachohusiana na uendelezaji wa shughuli yoyote ya ardhi bila kwanza kuripoti kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa au Kijiji hata kama umepewa kibali toka wilayani lengo ni kwanza kumfanya Mtendaji ajue ni kitu gani kinataka kufanywa kwenye mtaa wake lakini pia kama kweli kina baraka zote kisheria.
“Makamishna wa mikoa simamieni hili sababu lengo la serikali hapa ni kutaka kudhibiti ujenzi holela ndani ya miji na kuhakikisha kila kinachoendelezwa kipo kwenye taratibu za michoro ya mipango miji na kimefuata sheria hata kama eneo ni lake. Na hao watendaji watengeneze mtandao na wajumbe wao ndani ya serikali za mitaa ili kupeana taarifa nani anajenga wapi na kwa wakati gani,” alisisitiza Lukuvi.
Katika hilo aliagiza kila Mtendaji wa Mtaa apatiwe jedwali maalumu litakalokuwa na orodha ya kutambua wangapi kwenye mtaa wake wamemilikishwa ardhi kwa hati, na wanamiliki nini, nani anastahili kulipa kodi ya pango la ardhi, na zile hati wanazomiliki wameendeleza nini ijulikane!-azma ni kusaidia namna ya kuwakumbusha na kuchukua kodi kwenye maeneo hayo.
Hata hivyo, Lukuvi aliwataka maafisa ardhi wa wilaya kutoficha taarifa badala yake wahakikishe kila mmilikaji mpya wa ardhi anayepatikana ndani ya wilaya basi taarifa zote zinamfikia Mtendaji wa Mtaa husika, lengo ni pamoja na mambo mengine, kurahisisha uhakiki wa taarifa na utunzaji kumbukumbu katika muktadha wa kuwatambua wote wanaomiliki ardhi kwenye mitaa mbalimbali nchini.
Hata hivyo, Waziri alishauri vitolewe vipande vidogo-vidogo ndani ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi (Masterplan)kwa kila Manispaa na Halmashauri ‘Final Draft’ vinavyohusu mpango wa kila mtaa na akabidhiwe Mtendaji ili kumwezesha kuoanisha kama kinachoendelezwa kwenye ardhi kinafanana na mpango uliopo.
“Agizo na maelekezo haya nataka kabla ya bajeti yawe yametekelezwa na taarifa hizi ziwe mitaani kwa maana ya taarifa za wamilikishwaji wote kwenye mitaa ziwe zimeshapatikana na zipo kwa watendaji wa mitaa nchi nzima. Makamishna simamieni hili nitapita kukagua,” alisisitiza Lukuvi.
Katika hatua nyingine, akiwa wilayani Manyoni mbali ya kupongeza juhudi kubwa zilizofanyika katika mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye eneo la Masigati na Kinangali unapotekelezwa Mradi wa Kilimo cha Pamoja cha zao la Korosho kupitia mashamba makubwa (Block Farming), aliagiza wakulima wote wanaotekeleza mradi huo wapatiwe hati mara moja ili ziwasaidie kuweza kukopesheka.
Toa Maoni Yako:
0 comments: