Serikali inashauriwa kuwafukuza kazi walimu wanaofanya mapenzi na wanafunzi kama hatua moja muhimu ya kuepusha mimba mashuleni.


Walimu wanaotuhumiwa kufanya mapenzi na wanafunzi wakichukuliwa hatua za kinidhamu bila kuchelewa na habari za kufukuzwa kwao zikatangazwa hadharani itakuwa fundisho kwa walimu wengine kujiepusha na vitendo hivyo viovu.

Utafiti wa habari zinazochapishwa na magazeti kuhusu masuala ya mimba mashuleni uliofanywa na shirika hili unaoyesha kuwa katika kipindi cha miezi minne matukio 11 ya wanafunzi kupata ujauzito yalihusisha walimu.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba walimu wakuu wa shule za Msingi na Sekondari ni miongoni mwa walimu hao walioripotiwa kuhusika na matukio hayo ya aibu na ambapo katika tukio moja mwalimu aliyetuhumiwa kufanya mapenzi na wanafunzi aliuwawa.

Habari hizo za baadhi ya walimu kuwapa mimba wanafunzi au kufanya nao mapenzi ni miongoni mwa habari za elimu zilizochapishwa na magazeti kuanzia Desemba 2010 hadi mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu.

Walimu wamepewa dhamana kubwa ya kujenga na kutunza maadili mema kwa wanafunzi hivyo wakiwa ndio vinara kufanya mapenzi na mwanafunzi ni hatari na ni bora serikali impumzishe mwalimu atakayetuhumiwa au kubainika kwa kosa maana atakuwa amepoteza sifa ya kuwa mfano wa maadili ya kuigwa.

Tumeamua kutoa kwa umma habari hizi kuhusu mchango wa walimu katika tatizo la mimba mashuleni kutokana na kutambua kuwa walimu wananafasi muhimu na ya pekee katika kujenga mazingira ya kuzuia tatizo hilo.

Pia tunatambua kuwa kwa umma kuelewa kuwa kuna baadhi ya walimu ambao ni hatari kwa usalama wa wanafunzi, jamii itachukua hatua kwa kusaidiana na shule kuhakikisha walimu hao wanajulikana hadharani na hatua sahihi zinachukuliwa dhidi yao.

Tunapendekeza Wizaya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ifanye utafiti hasa kwa kuwahoji wanafunzi wa kike na wa kiume kuhusu tabia na mienendo ya walimu wao, bila shaka itaweza kupata taarifa za kulisaidia taifa kufahamu walimu wanachangiaje ukubwa wa tatizo la mimba mashuleni.

TAMWA tunavipongeza vyombo vya habari, wahariri na wanahabari kwa ujumla kwa kuzipa uzito habari zinazohusu elimu hasa tatizo la mimba mashuleni.

Tunaamini kuwa serikali, wizara husika, shule, walimu, wanafunzi, wanahabari na jamii kwa ujumla kila mmoja akiwa makini na kutekeleza wajibu wake kuzuia mimba mashuleni tatizo hili litapungua na taifa litapiga hatua kubwa ya maendeleo.

Tatizo la mimba mashuleni ni kubwa hapa nchini ambapo kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, katika kipindi cha miaka mitano, 2004-2008, jumla ya wanafunzi 28, 590 wakiwepo 11,599 wa sekondari na 16,991 wa shule za msingi, walikatisha masomo kwa kupata mimba.

Ananilea Nkya
Mkurugenzi Mtendaji.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: