Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kushiriki maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ‘Mei Mosi’ 2026 yaliyofanyika kimkoa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Grounds, jijini Dar es Salaam.
Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wakiwa katika ushiriki wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ‘Mei Mosi’ 2026 yaliyofanyika kimkoa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Grounds, jijini Dar es Salaam.
Bw. Mussa Lugembe, Mkurugenzi wa Kampasi ya Dar es Salaam, akizungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa niaba ya Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu.

Na Mwandishi Wetu.

Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) wakiwemo wa makao makuu na Kampasi ya Dar es Salaam, wameungana na wafanyakazi wengine kushiriki maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ‘Mei Mosi’ 2026 yaliyofanyika kimkoa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Grounds, jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, sekta binafsi pamoja na mashirika ya umma, yakilenga kutambua mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya taifa na kujadili masuala ya ustawi wao mahali pa kazi.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ambaye alitoa wito kwa wafanyakazi wote nchini kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na nidhamu kazini ili kulinda taswira ya serikali.

Akizungumza mbele ya mamia ya wafanyakazi waliojitokeza kusherehekea siku hiyo, Chalamila alisema kuwa wafanyakazi ndio sura halisi ya serikali kwa wananchi, hivyo wanapaswa kutambua uzito wa nafasi walizonazo katika kuhudumia jamii.

“Tunaposherehekea siku hii muhimu, ni vyema tukatambua kuwa mfanyakazi mmoja anaweza kufanya serikali ipendwe au ichukiwe. Hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kufanya kazi kwa uaminifu, bidii na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma,” alisema Chalamila.

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kuthamini mchango wa wafanyakazi na itaendelea kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi yao ili kuongeza tija na ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi.

Kwa upande wao, watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania walieleza kuwa ushiriki wao katika maadhimisho hayo ni sehemu ya kuonesha mshikamano na wafanyakazi wengine nchini pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha utumishi wa umma.

Maadhimisho ya Mei Mosi hufanyika kila mwaka duniani kote, yakilenga kuenzi mchango wa wafanyakazi na kuhamasisha haki, usawa na ustawi wao katika maeneo ya kazi. 

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: