Na Mwandishi Wetu

Zanzibar. Benki ya Exim Tanzania imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuchangia maendeleo ya jamii kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaojulikana kama Exim Cares, kwa kutekeleza miradi inayolenga kuboresha sekta za elimu, usalama, afya na uhifadhi wa mazingira.

Hatua hiyo imejidhihirisha visiwani Zanzibar kufuatia uzinduzi wa Tawi la Exim Bank Paje, ambapo benki hiyo imekabidhi samani za ofisi kwa Kituo kipya cha Polisi cha Paje na madawati 80 kwa Shule ya Msingi Paje, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za jamii sambamba na kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi.

Mchango huo unakuja wakati ambapo eneo la Paje linaendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa shughuli za utalii, biashara na ongezeko la idadi ya watu, hali inayoongeza mahitaji ya huduma bora za kijamii na taasisi imara za umma. Kwa kuchangia vifaa vya ofisi katika kituo hicho cha polisi, Exim Bank inalenga kusaidia utoaji wa huduma bora za usalama kwa wakazi wa Paje na maeneo ya jirani.

Mbali na kuimarisha usalama, benki hiyo imewekeza pia katika sekta ya elimu kwa kutoa madawati 80 kwa Shule ya Msingi Paje. Madawati hayo yanatarajiwa kunufaisha zaidi ya wanafunzi 250 kila mwaka kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza changamoto ya uhaba wa samani shuleni.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Mhe. Othman Ali Maulid(kushoto) akipokea moja ya dawati kati ya madawati 80 kutoka kwa Mkuu wa Idara Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania(kulia) ikiwa kama ishara ta benki hiyo ya kurudisha kwa jamii chini ya progamu yao ya Exim Care. Tukio hili limefanyika tarehe 26 juni 2026, visiwani Zanzibar.
---
Uwekezaji huo unaaminika kuongeza ari ya kujifunza kwa wanafunzi pamoja na kuwawezesha walimu kufundisha katika mazingira bora zaidi, hatua inayochangia kuboresha ubora wa elimu kwa muda mrefu.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Exim Bank Tanzania, Stanley Kafu, alisema benki hiyo inaamini maendeleo ya kweli hayawezi kupimwa kwa mafanikio ya kifedha pekee, bali pia kwa mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi.

"Katika Benki ya Exim Tanzania tunaamini kuwekeza katika jamii ni msingi wa maendeleo endelevu. Elimu na miundombinu ya jamii ni nguzo muhimu za maendeleo, na tumejizatiti kuunga mkono miradi inayozalisha matokeo yenye maana na athari za kudumu kwa watu tunaowahudumia," alisema Kafu.
Alieleza kuwa uwekezaji katika elimu ni uwekezaji katika kizazi kijacho, huku akisisitiza kuwa kuboresha mazingira ya kujifunzia kunawawezesha watoto kupata elimu bora na kuwa sehemu ya nguvu kazi itakayochochea maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Exim Bank, miradi hiyo ni sehemu ya mkakati wake mpana wa Uwajibikaji kwa Jamii unaolenga kujenga ushirikiano wa muda mrefu na jamii kupitia uwekezaji katika elimu, afya, uwezeshaji wa jamii na maendeleo endelevu.

Benki hiyo imeeleza kuwa kufunguliwa kwa Tawi la Paje siyo tu hatua ya kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi, bali pia ni mwanzo wa ushirikiano wa kudumu na jamii ya Zanzibar kupitia miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.

Kupitia mpango wa Exim Cares, benki hiyo imeendelea kuonesha kuwa taasisi za kifedha zina nafasi muhimu katika kuchochea maendeleo ya kijamii, huku mafanikio yake yakipimwa si kwa ukuaji wa biashara pekee, bali pia kwa mchango wake katika kuboresha maisha ya watu na jamii zinazoizunguka.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: