
Dar es Salaam. Kampuni ya Puma Energy Tanzania imekabidhi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania gawio la kihistoria la shilingi bilioni 15, ikiwa ni gawio kubwa zaidi kuwahi kutolewa na kampuni hiyo tangu kuanzishwa kwake. Gawio hilo linawakilisha nusu ya faida iliyopatikana na kampuni, huku likionyesha mafanikio ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kupitia umiliki wa pamoja wa hisa, ambapo Serikali inamiliki asilimia 50 ya kampuni hiyo.
Hafla ya makabidhiano ilifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo hundi hiyo ilipokelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mbele ya viongozi wa Serikali, Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Puma Energy Tanzania. Gawio hilo limeongezeka kwa asilimia 11 ikilinganishwa na shilingi bilioni 13.5 zilizotolewa mwaka 2025, hatua inayodhihirisha kuimarika kwa utendaji wa kampuni na mafanikio ya uwekezaji wake nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia aliipongeza Puma Energy Tanzania pamoja na makampuni mengine yanayotekeleza wajibu wao kwa Serikali, akisema mchango wao unaimarisha uchumi wa taifa na kuthibitisha manufaa ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kukuza maendeleo ya nchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Puma Energy Tanzania, Balozi George Madafa, alisema gawio hilo linaonyesha uimara wa biashara ya kampuni na mafanikio ya mkakati wake wa ukuaji wa muda mrefu. Alisema kampuni itaendelea kuzalisha thamani kwa wanahisa wake huku ikichangia maendeleo ya taifa kupitia gawio, kodi, uwekezaji na uundaji wa ajira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, alisema kampuni imeendelea kuwekeza katika kupanua mtandao wa vituo vya mafuta, huduma za mafuta ya ndege, biashara ya gesi ya LPG na matumizi ya nishati safi kupitia Gesi Asilia Iliyobanwa (CNG). Alisema uwekezaji huo unaunga mkono ajenda ya Serikali ya maendeleo ya viwanda na matumizi ya nishati safi, huku ukiimarisha upatikanaji wa huduma za nishati nchini.Fatma alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Puma Energy Tanzania imechangia zaidi ya shilingi trilioni 1.4 kupitia kodi na tozo mbalimbali kwa Serikali. Aidha, alisema kampuni hiyo imetambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na rekodi yake bora ya ulipaji kodi na mchango wake katika kuongeza mapato ya Serikali.
Kwa sasa, Puma Energy Tanzania inaendesha zaidi ya vituo 100 vya huduma za mafuta nchini, kituo kikubwa cha kuhifadhi mafuta pamoja na maghala katika maeneo mbalimbali. Kampuni pia husambaza mafuta ya ndege katika viwanja vinane vya ndege, ikiwemo viwanja vyote vya kimataifa nchini, na inaongoza katika matumizi ya nishati safi kupitia Kituo Kikuu cha CNG kikubwa zaidi barani Afrika pamoja na mtandao unaoendelea kupanuka wa vituo vya CNG jijini Dar es Salaam na Morogoro.
Mbali na biashara ya mafuta, kampuni inaendelea kupanua upatikanaji wa gesi ya kupikia kupitia Puma Gas, huku ikiendeleza biashara ya vilainishi na maduka ya Shop Express yanayowapatia wateja bidhaa na huduma mbalimbali. Uwekezaji huo unaendelea kuifanya Puma Energy kuwa miongoni mwa kampuni zinazoongoza katika kuchochea maendeleo ya sekta ya nishati na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.


Toa Maoni Yako:
0 comments: