Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kufanyia kazi kwa kina hoja zote zilizowasilishwa na wafanyakazi nchini, zilizotolewa katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika leo.

Rais Samia ametoa maelekezo hayo akiwa Mgeni Rasmi wa maadhimisho hayo yaliyofanyika leo mkoani Njombe, ambapo amesisitiza umuhimu wa serikali kuzipokea na kuzifanyia kazi hoja hizo kwa umakini ili kuendelea kulinda na kuimarisha hadhi, haki na maslahi ya wafanyakazi nchini.

Amesema kuwa wafanyakazi ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa, hivyo serikali haina budi kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa njia ya majadiliano na utekelezaji wenye tija.

Katika hotuba yake, Rais Samia pia amewataka wafanyakazi kujiandaa kukabiliana na mabadiliko ya dunia ya sasa, ikiwemo mageuzi ya kiuchumi na kiteknolojia ambayo yanaathiri soko la ajira na namna ya utoaji wa huduma kazini.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani, ushirikiano na kuaminiana miongoni mwa wananchi na wafanyakazi, akibainisha kuwa misingi hiyo ndiyo mhimili mkuu wa maendeleo na ustawi wa taifa.

Hata hivyo Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na vyama vya wafanyakazi pamoja na wadau wa ajira nchini ili kuhakikisha changamoto zinazojitokeza kazini zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu. Amesema lengo la serikali ni kujenga mazingira bora ya kazi yanayochochea tija, nidhamu na uzalishaji, huku haki za wafanyakazi zikiendelea kulindwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo nchini.

Amesema endapo mshikamano na utulivu vitaendelea kudumishwa, Tanzania itaendelea kuwa nchi salama, yenye maendeleo endelevu na mazingira bora ya kazi kwa wananchi wake wote.


Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: