Kituo cha wanyamapori cha Serval Wildlife kimetoa tamko rasmi kufuatia taarifa za kifo cha mwanahabari na mtengeneza maudhui mtandaoni, Ashley, kikieleza masikitiko yake na kufafanua kuhusu tukio hilo lililozua mjadala mkubwa mitandaoni.
Kupitia taarifa hiyo, Serval Wildlife ilieleza kuwa inatoa pole za dhati kwa familia, ndugu na marafiki wa marehemu, ikisisitiza kuwa wako pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
Aidha, taasisi hiyo imeweka wazi kuwa tukio la kifo hicho halikutokea katika eneo lao, bali lilitokea visiwani Zanzibar, jambo lililothibitishwa pia na Zanzibar Police Force kupitia taarifa yao rasmi.
Serval Wildlife imefafanua kuwa marehemu Ashley aliwahi kutembelea kituo hicho na kupata uzoefu mzuri, huku akiondoka katika hali njema. Imeongeza kuwa video zinazosambaa mtandaoni kwa sasa zinatokana na ziara yake katika kituo hicho, hali iliyosababisha mkanganyiko kuhusu eneo halisi la tukio.
Katika hatua nyingine, taasisi hiyo imesema haitashiriki wala kuchapisha tena picha au video za marehemu kwenye kurasa zake, kwa heshima na kuepuka kuonekana kama inatumia tukio hilo kwa masoko.
Tamko hilo limehitimishwa kwa kuomba uelewa kutoka kwa umma pamoja na kuendelea kuiombea familia ya marehemu katika kipindi hiki cha majonzi.



Toa Maoni Yako:
0 comments: