Dodoma Desemba 26, 2025: Serikali imeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu mwenendo wa utoaji wa huduma katika Hospitali ya Temeke, ikiwemo kuzimwa kwa mashine ya X-Ray, baada ya kupokea taarifa za madai ya rushwa na ukiukwaji wa maadili ya kazi miongoni mwa baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa Desemba 26, 2025 na Wizara ya Afya, ufuatiliaji uliofanywa umebaini uwepo wa vitendo vya rushwa ambapo baadhi ya wahudumu wa afya walidaiwa kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa waliowahonga kwanza huku wengine wakinyimwa haki yao ya kupata matibabu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa vitendo hivyo vimesababisha wagonjwa kadhaa kukosa huduma stahiki, pamoja na kuwakashifu baadhi ya watumishi waliodaiwa kuwafokea wagonjwa na kudharau maadili ya taaluma yao.
Kufuatia hali hiyo, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, kufanya uchunguzi wa kina katika hospitali hiyo ili kubaini chanzo cha matatizo hayo na kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wote watakaobainika kuhusika na vitendo vya rushwa au uzembe.
Aidha, Waziri Mchengerwa ametoa onyo kali kwa watumishi wote wa sekta ya afya nchini, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya mtumishi yeyote atakayekiuka maadili ya kazi, kujihusisha na rushwa au kushindwa kuwahudumia wananchi kwa haki na utu.
Serikali imewahakikishia wananchi kuwa inaendelea kusimamia utoaji wa huduma bora za afya na kuchukua hatua stahiki ili kurejesha imani ya wananchi katika taasisi za huduma za afya.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, John Mapepele.



Toa Maoni Yako:
0 comments: