Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari Machumu akizungumza na Waandishi wa Habari wa Mtandaoni pamoja na Wanablogu mbalimbali, Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujitambulisha na kupokea maoni yao, ikiwa ni mfululizo wa mikutano na wadau wa Tasnia ya Habari kwa ajili ya kuboresha masuala mbalimbali ya Mawasiliano baina ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu na Vyombo vya Habari, tarehe 27 Novemba, 2025.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) umetolea ufafanuzi taarifa zinazozagaa mtandaoni zikidai kuwa wanahabari wa maudhui ya mtandaoni waliitwa Ikulu kwa ajili ya kupewa maelekezo kuhusu maandamano yanayodaiwa kufanyika Desemba 9. TBN imetaja madai hayo kuwa ya uongo, yasiyo na ushahidi na yenye lengo la kupotosha umma.

Katika taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, mtandao huo ulifafanua kuwa mkutano huo uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam ulikuwa mahsusi kwa ajili ya utambulisho wa Mkurugenzi mpya wa Mawasiliano Ikulu, Bw. Bakari Machumu, kwa wadau wa sekta ya habari, wakiwemo wanahabari wa maudhui ya mtandaoni.
“Kikao hicho kilikuwa cha utambulisho na kuweka msingi wa ushirikiano kati ya ofisi ya Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu na wadau wa habari. Hakukuwa na ajenda yoyote ya siri wala maelekezo kuhusu maandamano,” alisema Msimbe.

TBN ililaani kitendo cha kusambazwa kwa kipande kifupi cha video ya mkutano huo na baadhi ya watu, akiwemo wanasiasa, kwa madai kwamba kililenga kujenga taswira potofu na kuchochea taharuki. Msimbe alisema hatua kama hizo zinaharibu tasnia ya habari na kupunguza uaminifu katika mijadala ya kitaifa.

“Ni muhimu kwa wadau na wananchi kujenga tabia ya kuthibitisha taarifa kabla ya kuzisambaza. Upotoshaji wa aina hii hauisaidii jamii na unaweza kuchochea mgawanyiko,” aliongeza.

TBN ilimpongeza Bw. Machumu kwa kuonesha utayari wa kufanya kazi kwa karibu na wadau wa habari na ikamsihi kuendelea na utendaji wa uwazi na mawasiliano yenye tija.

Wananchi wametakiwa kutanguliza hekima, uzalendo na uhalisia wa taarifa ili kulinda amani na kuimarisha maadili katika matumizi ya mitandao ya kijamii.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: