Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto akiangalia bidhaa za Wajasiriamali wa Tanzania katika alipotembelea Maonesho ya 25 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali, yanayofanyika Nairobi, Kenya tarehe 11 Novemba, 2025 wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo.

Na OWM (KVAU) – Nairobi

Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto, amepongeza wajasiriamali wa Tanzania kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora, ubunifu na ushindani mkubwa, alipokuwa akitembelea mabanda ya Watanzania katika Maonesho ya 25 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Nguvu Kazi/Jua Kali) yanayoendelea jijini Nairobi, Kenya.

Akizungumza Novemba 11, 2025, wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo, Rais Ruto alisema anavutiwa na namna Watanzania wanavyotumia ubunifu wao kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi viwango vya kikanda na kimataifa.

“Wajasiriamali wa Tanzania mmeonesha mfano bora wa ubunifu na ubora wa kazi. Ni wakati sasa wa kuimarisha ushirikiano kati ya Kenya, Tanzania na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuongeza uzalishaji na kupanua masoko,” alisema Rais Ruto.
Ameongeza kuwa dhamira ya viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha vinavyozuia biashara mipakani, ili kuwezesha ukuaji wa uchumi na ajira kwa vijana.
 
Maonesho yawanufaisha Wajasiriamali

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM), Bi. Alana Nchimbi, alisema maonesho hayo yamekuwa chachu ya maendeleo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati wanaojihusisha na sekta isiyo rasmi.

“Kupitia maonesho haya, wajasiriamali wamepata fursa ya kurasimisha shughuli zao, kutangaza bidhaa, kubadilishana ujuzi na kupata masoko mapya ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Nchimbi.
Wajasiriamali wafurahia pongezi

Wajasiriamali wa Tanzania walionyesha furaha kubwa kufuatia pongezi hizo kutoka kwa Rais Ruto, wakisema zinawapa motisha kuendelea kuboresha bidhaa zao na kupanua biashara zao nje ya mipaka ya Tanzania.

“Tumejifunza mengi kutoka kwa wenzao wa nchi nyingine, tumeona masoko mapya na tumejipanga kutumia fursa hii kuinua bidhaa zetu,” alisema mmoja wa wajasiriamali hao.

Maonesho hayo ya Nguvu Kazi/Jua Kali yamekusanya wajasiriamali kutoka nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, yakiwa na lengo la kukuza ushirikiano, ubunifu na maendeleo ya viwanda vidogo barani Afrika.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: