Na Mwandishi Wetu. 

Dodoma, Septemba 18, 2025 – Mgombea urais kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, ameibua upya mjadala wa kisiasa baada ya kufungua shauri Mahakama Kuu akiwashitaki Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Shauri hilo linahusu uamuzi wa kumkata jina lake kwenye orodha ya wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, hatua ambayo anadai haikufuata taratibu za kisheria na imekiuka haki yake ya kikatiba.

Katika hati ya madai aliyowasilisha kortini kupitia wakili wake Jasper Sabuni, Mpina ameeleza kuwa maamuzi ya Msajili yalifanyika kwa upendeleo na bila kuzingatia misingi ya haki, hivyo kuathiri nafasi yake kisiasa na kidemokrasia. Ameomba mahakama itengue uamuzi huo na kuamuru jina lake lirejeshwe katika mchakato wa uchaguzi.

Safari ya mgogoro wa Mpina

Safari ya Mpina kuelekea kugombea urais imekuwa na misukosuko mikubwa. Baada ya kuchukua fomu ndani ya ACT-Wazalendo, jina lake liliwekewa pingamizi na wanachama wenzake likidai hakuwa na sifa zinazohitajika.

Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ilitupilia mbali pingamizi la awali na kumtangaza kuwa mgombea halali pamoja na mgombea mwenza wake, Fatma Fereji. Baada ya hatua hiyo, Mpina alirudisha fomu zake lakini akakataa kupokea gari la kampeni alilopewa na tume, akisisitiza kwamba chama chake kipo tayari kujitegemea.

Hata hivyo, mnamo Agosti 26, 2025, jina lake liliondolewa kwenye orodha ya wagombea, uamuzi alioupinga mahakamani. Mnamo Septemba 11, 2025, Mahakama Kuu Masijala Kuu Dodoma iliamuru INEC kumrejesha katika mchakato wa uteuzi.

Baada ya kurejeshwa na kutangazwa tena rasmi mnamo Septemba 13, 2025, jina lake lilipelekwa tena kwenye tume na kufutwa kwa mara ya pili, safari hii kufuatia pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wanachama wengine.

Sakata la Monalisa

Katika hatua iliyoibua mjadala zaidi, kikao cha Kamati ya Uongozi wa ACT-Wazalendo kilimvua uanachama mwanachama wa chama hicho, Monalisa Joseph Ndala, baada ya kuwasilisha malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa yaliyosababisha kuenguliwa kwa Mpina.

Monalisa alilalamika kuwa Mpina alipata uanachama wa ACT-Wazalendo tarehe 5 Agosti 2025, nje ya muda wa kikatiba uliopangwa, ambao ulipaswa kuwa kabla ya 25 Mei 2025. Msajili wa Vyama vya Siasa alikubaliana na hoja hizo na kuzifikisha INEC, hatua iliyosababisha jina la Mpina kufutwa kwenye orodha ya wagombea.

Katika taarifa iliyotiwa saini na Katibu wa Tawi la Mafifi mkoani Iringa, Neema Ernest Kivamba, chama kilieleza kuwa Monalisa amepoteza sifa za uanachama kwa kushindwa kutekeleza matakwa ya katiba ya chama.

“Kuanzia leo tarehe 28.08.2025, Kamati ya Uongozi ya Tawi la Mafifi imekuondoa katika orodha ya wanachama wake. Kadi namba 0000245 iliyokuwa imeandikishwa kwa jina lako ipo wazi na tumeitaarifu Idara ya Oganaizisheni, Uchaguzi na Wanachama wa Chama Taifa ili iweze kutolewa kwa mwanachama mwengine,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kauli ya Mpina

Akizungumza baada ya kufungua kesi, Mpina alisema hatua yake inalenga kulinda siyo tu haki yake binafsi, bali pia misingi ya kidemokrasia nchini.

“Huu siyo mgogoro wangu pekee, bali ni vita ya kulinda misingi ya katiba na demokrasia ya vyama vingi nchini kwetu,” alisema.

Matarajio

Kesi hiyo imeibua mijadala mikubwa katika medani za kisiasa, huku wadau mbalimbali wakisubiri kuona iwapo mahakama itatoa uamuzi utakaoweza kubadilisha taswira ya mchakato wa uchaguzi wa mwaka huu, au kama itakuwa mwisho wa safari ya Mpina kuelekea Ikulu.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: