Na Oscar Assenga, Tanga

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwasili mkoani Tanga Septemba 28, 2025, kwa ajili ya ziara ya kampeni ya siku tatu, ambapo atapokelewa katika eneo la Mkata, wilayani Handeni kabla ya kuelekea Tanga mjini kwa mapumziko.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Alhaj Rajab Abdurhaman, alisema Dkt. Samia ataanza ratiba yake ya kampeni kwa mkutano wa hadhara wilayani Pangani, kisha ataendelea na mikutano mingine Tanga mjini na maeneo mengine ya mkoa.

“Niwaombe wananchi na wana CCM wote kujitokeza kwa wingi kumlaki mgombea wetu wa urais, kwani ndiye chaguo letu kupitia ilani ya uchaguzi ya 2025/2030,” alisema Abdurhaman.

Wananchi watakiwa kujitokeza kwa wingi

Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa wananchi katika maeneo yote ambayo Dkt. Samia atapita wanapaswa kuonyesha mshikamano kwa kujitokeza kwa wingi, kwani anakuja kuzungumza nao moja kwa moja kuhusu ilani ya CCM na mipango ya maendeleo kwa miaka mitano ijayo.

Tanga yatajiona yenye bahati

Alhaj Rajab, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu (MCC), alisema mkoa wa Tanga ni miongoni mwa wenye bahati, kwani hii ni mara ya pili katika kipindi cha mwaka mmoja kupokea ugeni wa Dkt. Samia – mara ya kwanza akiwa katika ziara ya kikazi miezi michache iliyopita.

“Tulipompokea kwa ziara ya kikazi, miradi mingi ya maendeleo ilifunguka na kusonga mbele. Kwa mfano, kasi ya ujenzi wa barabara ya Tanga–Sadani–Bagamoyo imeongezeka, vivyo hivyo barabara ya Soni–Bumbuli–Dindira hadi Korogwe kupitia Meta imepangwa kuanza muda si mrefu,” alisema.

Imani ya wananchi

Aidha, alisema wananchi wa Tanga wana matumaini makubwa na CCM kwa sababu chama hicho kimekuwa kikiahidi na kutekeleza kwa vitendo miradi ya maendeleo, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia.

“Tunamwamini Dkt. Samia kwa sababu ametupa matumaini makubwa. Ametumia hekima na busara kulinda amani ya nchi na pia kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo. Tuna uhakika wananchi watampa kura nyingi,” aliongeza.

Ziara hiyo ya kampeni inatarajiwa kugusa wilaya za Muheza na Korogwe, huku ratiba kamili ya maeneo mengine ikitarajiwa kutolewa na chama kwa wakati muafaka.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: