Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ametaja vipaumbele vikuu atakavyovishughulikia ndani ya siku 100 za kwanza za Serikali yake iwapo atachaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi waliofurika Uwanja wa Tanganyika Peckers jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM, Dk. Samia alibainisha kuwa Serikali yake itaanza kwa kuweka msingi wa huduma za afya, elimu, ajira na uboreshaji wa mazingira ya biashara.
Huduma za Afya kwa Wote
Dk. Samia aliahidi kuanza utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kwa awamu ya majaribio, ikianzia kwa wajawazito, watoto na wazee. Alisisitiza kuwa huduma hizo zitagharamiwa na Serikali kupitia mfuko wa bima ya afya.
Vilevile, Serikali yake itapiga marufuku hospitali zote nchini kuzuia miili ya marehemu kutokana na madeni ya matibabu, badala yake ndugu watalipa kwa utaratibu maalum bila kuchelewesha mazishi.
“Tutahakikisha vipimo vya magonjwa ya moyo, figo, mishipa ya fahamu, mifupa na kisukari vinatolewa bure kwa wananchi wasiokuwa na uwezo. Pia, ndani ya siku 100 tutatoa ajira 5,000 katika sekta ya afya wakiwemo wauguzi na wakunga,” alisema Dk. Samia.
Elimu na Ajira Mpya
Katika sekta ya elimu, Rais Samia aliahidi kuhakikisha kila mtoto wa darasa la tatu anakuwa na uwezo wa kusoma na kuandika vizuri. Pia alisema Serikali itaajiri walimu 7,000 wa hisabati na sayansi ili kuimarisha elimu ya kisayansi.
Kwa upande wa ajira na uwezeshaji, Dk. Samia alisema Serikali itatenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kutoa mitaji kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, kurasimisha mama lishe, bodaboda na wajasiriamali wengine wadogo ili kuingizwa katika mfumo rasmi wa Serikali.
Mazingira ya Biashara na Viwanda
Alibainisha kuwa Serikali yake itaanzisha programu ya mitaa ya viwanda wilayani ili kuzalisha ajira kupitia mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, madini na misitu.
Pia, itazindua mpango wa pamoja kati ya vyuo vya ufundi, vyuo vikuu na waajiri kwa lengo la kuhakikisha wahitimu wanapata nafasi ya vitendo viwandani.
Maji na Nishati Safi
Dk. Samia aliahidi kuanza ujenzi wa “Gridi ya Taifa ya Maji” itakayounganisha vyanzo vikuu vya maji ikiwemo Ziwa Victoria, Tanganyika, Nyasa na mito mikubwa. Lengo ni kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika nchini.
Aliongeza kuwa Serikali itaendeleza jitihada za kusambaza nishati safi ya kupikia ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Uwajibikaji na Katiba Mpya
Katika kusimamia uwajibikaji, Dk. Samia alisema mawaziri na wakuu wa mikoa watatakiwa kutoa taarifa na kujibu maswali ya wananchi kwa njia ya simu.
Aidha, aliahidi kuendeleza mashauriano na wadau wa siasa, sekta binafsi na taasisi za kiraia, sambamba na kuunda tume maalum ya maandalizi ya mchakato wa Katiba Mpya.



Toa Maoni Yako:
0 comments: