Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule, ameipongeza Tume ya Madini kwa kazi nzuri ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu fursa za kiuchumi zilizopo katika Sekta ya Madini kupitia banda lake la maonesho katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo tarehe 5 Agosti 2025, Mhe. Senyamule alisema Tume ya Madini imekuwa mfano wa kuigwa kwa taasisi za umma kwa namna inavyotekeleza majukumu yake kwa vitendo, hususan katika kuonesha mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa nchi..
"Nawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya. Mnaendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchimbaji, uongezaji thamani madini, na biashara ya madini kupitia masoko ya madini yaliyoanzishwa," alisema Senyamule.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alibainisha kuwa mkoa wa Dodoma umejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi za madini yakiwemo ya viwandani, vito, na ujenzi. Alisisitiza umuhimu wa kuhamasisha uwekezaji zaidi kwenye sekta hiyo kwa kutumia sera na sheria rafiki zilizopo kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Kwa upande wao, Maafisa wa Tume ya Madini waliopo kwenye banda hilo walieleza kuwa taasisi hiyo itaendelea na dhamira ya kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo wa shughuli za madini. Hii ni pamoja na kupata leseni, kutumia teknolojia ya kisasa kuongeza thamani ya madini, pamoja na kuhakikisha madini yote yanauzwa kupitia masoko rasmi yaliyowekwa.

Maonesho ya Nane Nane mwaka 2025 yanaendelea kujikita katika kuonesha mafanikio ya sekta za kilimo, mifugo, viwanda na madini, huku Tume ya Madini ikitajwa kuwa miongoni mwa taasisi zinazovutia maelfu ya wananchi kutokana na ubunifu wake katika kuelimisha na kutoa taarifa muhimu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: