Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema wakulima wa ufuta, mbaazi na korosho wamenufaika na mfumo wa stakabadhi ghalani, uliowawezesha kupata zaidi ya shilingi bilioni 11 kutokana na mauzo ya mazao hayo.
Akizungumza na wananchi wa Morogoro, Dkt. Samia alisema: “Tutahakikisha sekta ya mifugo inaimarika kwa kujenga mashamba darasa 15 ya malisho na uzalishaji. Vilevile, serikali itatoa shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya mikopo ya wajasiriamali 7,015 kupitia halmashauri.”
Aidha, alieleza kuwa vijiji 149 na vitongoji 417 vimepatiwa umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA). “Huduma hii ya nishati ni chachu ya maendeleo vijijini na tutaendelea kusambaza hadi maeneo yote kufikiwa,” aliongeza.
Kuhusu miundombinu, Dkt. Samia aliahidi kujenga barabara ya Bigwa–Kisaki kwa kiwango cha lami baada ya ombi la mgombea ubunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale (Babu Tale). “Barabara hii ni muhimu kwa usafirishaji wa mazao na huduma, na tutahakikisha inatekelezwa,” alisema.
Akihitimisha, Dkt. Samia aliwaomba wananchi kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 pamoja na wagombea wa CCM. “Niwaombe siku ya kupiga kura mkachague Chama Cha Mapinduzi, mkanipigie mimi, wabunge na madiwani wa CCM. Wale jamaa zangu wameweka mpira kwapani, basi kazi ni kwenu wananchi kutuwezesha kushinda,” alisema huku akihimiza viongozi wa chama kutumia baiskeli na pikipiki walizopewa kufanikisha kampeni.




.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments: