Na Mwandishi Wetu.

DAR ES SALAAM – Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata shehena kubwa ya dawa mpya ya kulevya aina ya Mitragyna Speciosa yenye uzito wa tani 18.5, iliyokuwa ikiingizwa nchini kutoka Sri Lanka kwa kufichwa kama mbolea.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema jana Agosti 13, 2025 kuwa shehena hiyo, iliyohifadhiwa kwenye kontena lenye ukubwa wa futi 40, ilikuwa na jumla ya mifuko 756 yenye uzito wa kilo 18,485.6.

Katika tukio hilo, watuhumiwa saba walikamatwa akiwemo raia wawili wa Sri Lanka – Jagath Prasanna Madduma Wellalage (46) na Santhush Ruminda Hewage (25) – pamoja na Watanzania watano.

“Hii ni mara ya pili kukamatwa kwa aina hii ya dawa nchini. Mwezi Juni tulikamata mifuko 450 yenye tani 11.5 za dawa hiyo hiyo, hivyo kwa pamoja tumekamata zaidi ya tani 30 ndani ya kipindi kifupi,” alisema Lyimo.

Alieleza kuwa Mitragyna Speciosa, inayotokana na mmea unaofahamika kama Kratom na kupatikana zaidi Kusini Mashariki mwa Asia, ina madhara sawa na dawa za kulevya jamii ya Afyuni kama Heroin na Morphine, ikiwemo kuathiri mfumo wa fahamu, kusababisha uraibu na hata vifo vya ghafla.

Lyimo alisema ukamataji huo unaonyesha changamoto mpya katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini na kuahidi kuimarisha ufuatiliaji, udhibiti na kuvunja mitandao ya biashara haramu ya dawa hizo.

Aliongeza kuwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kiafya, kijamii na kiuchumi, hivyo DCEA itaendeleza operesheni za nchi nzima pamoja na kuongeza wigo wa elimu kwa umma ili kulinda nguvu kazi ya taifa na kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: