UFAFANUZI WA TET

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) inaushukuru umma kwa kuendelea kufuatilia kwa karibu taarifa mbalimbali zinazozuhusu utekelezaji wa majukumu yake. TET imeendelea kuhakikisha kuwa majukumu yake yote kama yalivyobainishwa katika sheria anzilishi yanatekelezwa kwa ubora na kuwa yanachangia katika kuimarisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha utoaji wa elimu na hatimaye kupelekea kuwa na wahitimu wenye ujuzi wa kuajiriwa, kujiari na kuajiri wengine.

Aidha katika kuhakikisha hili, TET imeendelea kupokea maswali, maoni na ushauri kutoka kwa wadau kwa lengo la kuhakikisha kuwa majukumu yake yanatekelezwa kwa kiwango cha juu.

TET imepokea maoni ya mdau yaliyotolewa kupitia mtandao wa kijamii wa JamiiForums kuhusu somo tajwa hapo juu na inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao kwa umma:

Utekelezaji wa Majukumu kwa Wakati
Utekelezaji wa Mtaala wa Kidato cha Tano na Sita uliahirishwa kwa sababu ambazo zilibainishwa wazi kwa umma. Aidha, kuhairishwa kwa utekelezaji wa mtaala huo hakukuwa na athari katika ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi husika. Katika Mwaka wa Fedha 2024/25 TET imesambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa wakati. Aidha, vifaa hivyo pia vimesambazwa katika Maktaba Mtandao ya TET inayopatikana bure kupitia anwani Ol.tie.go.tz. Kazi ya kusambaza vifaa hivi ni endelevu na juhudi za kujazia upungufu pale unapotokea ni endelevu.

Kuhusu Mafunzo ya Walimu
TET inatambua na kuthamini kuwa walimu walioko kazini tayari walipata mafunzo ya muda mrefu yanayojulikana kwa Kiingereza kama Pre-service ambayo yaliwawezesha kuwa na uelewa mkubwa wa maudhui ya masomo wanayofundisha.

Pamoja na mafunzo haya ya awali Serikali inatambua na kuthamini umuhimu wa mafunzo ya mara kwa mara kwa walimu yenye lengo la kuwafanya kuwa wapya na kuwawezesha kwenda na wakati katika mbinu za ufundishaji na ujifunzaji.

Hivyo, lengo la mafunzo yaliyotolewa kwa walimu wa Kidato cha Tano liikuwa ni kutoa uelewa juu ya masuala yaliyoboreshwa katika mtaala wa Mwaka 2023. Ili kuyafanya mafunzo kuwa endelevu, serikali imeanzisha utaratibu wa kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini unaojulikana kama MEWAKA. Mafunzo haya hutolewa katika ngazi ya shule katika siku moja ya kila wiki.

Malipo ya Posho kwa Walimu
TET inatambua mchango na umuhimu wa walimu katika utekelezaji wa mtaala. Hata hivyo ni muhimu kukumbuka kuwa, malipo ya posho huhusisha kuwasilisha taarifa sahihi za kibenki kabla ya kufanyika kwa malipo husika. Kwa bahati mbaya baadhi ya walimu hawakuwasilisha taarifa sahihi na hivyo kupelekea ucheleweshaji wa malipo yao.

Baada ya hili kugundulika, TET ilifanya mawasiliano na walengwa na wahusika walirekebisha taarifa zao na malipo husika yalifanyika. Kwa bahati mbaya, baadhi ya walimu walichelewa kurekebisha taarifa zao na ikapelekea kufikia mwisho wa Mwaka wa Fedha.

Orodha ya walimu ambao malipo yao yalikuwa bado kukamilika ipo na malipo yao yatafanyika mara baada ya taratibu za kiserikali za kufunga na kuanza mwaka mpya wa fedha kukamilika.

TET inawashukuru umma unaofuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa majukumu yake. Aidha, tunaendelea kupokea maoni na ushauri kutoka kwa wadau wote. Maoni hayo yatafanyiwa kazi ili kuhakikisha kuwa utendaji wa TET unakuwa wa tija na unapelekea kuwa na matokeo chanya. Kwa maoni na ushauri wasiliana nasi kupitia barua pepe director.general@tie.go.tz

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET)
10 Julai 2025
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: