
Na Mwandishi Wetu, Arusha
Afisa Rasilimali Watu Mwandamizi kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Bi. Shukrani J. Haule, amekabidhiwa Tuzo ya Mfanyakazi Hodari wa Taasisi kwa mwaka 2025 kutokana na mchango wake mahiri katika usimamizi wa rasilimali watu ndani ya taasisi hiyo ya serikali.
Tuzo hiyo imetolewa leo, Julai 23, 2025, jijini Arusha katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC, wakati wa Mkutano wa Jumuiya ya Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala katika Utumishi wa Umma Tanzania (TAPA-HR). Bi. Shukrani amekabidhiwa tuzo hiyo na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said.
Mkutano huo mkubwa umehudhuriwa na wataalamu zaidi ya 900 kutoka katika Wakala wa Serikali, Wizara, Taasisi za Umma, Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Washiriki hao wamekusanyika kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, mbinu bora na mikakati ya kuboresha sekta ya rasilimali watu na utawala katika utumishi wa umma nchini.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Bi. Shukrani ameishukuru NEMC kwa kumuamini na kumpa majukumu ambayo yamewezesha kuonyesha weledi na uwezo wake kazini. Amesema kuwa tuzo hiyo ni chachu ya kuongeza juhudi katika kuwahudumia watumishi kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya haki, usawa na maendeleo ya kitaasisi.
Kwa upande wake, uongozi wa NEMC umepongeza mafanikio hayo ya Bi. Shukrani na kueleza kuwa ushindi huo ni kielelezo cha dhamira ya taasisi hiyo ya kuendeleza watumishi wake na kuimarisha utendaji kwa maslahi ya umma na maendeleo ya taifa.
Tuzo hiyo inaakisi juhudi za serikali katika kutambua na kuthamini wafanyakazi wa umma wanaofanya kazi kwa bidii, uadilifu na ubunifu katika taasisi zao.



Toa Maoni Yako:
0 comments: