Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha.

Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro imeahidi kuanza kutenga bajeti sambamba na kuwashirikisha katika vikao, mikutano na shughuli nyinginezo Waratibu wa Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) ngazi ya Wilaya ili kusaidia sekta zote kuona umuhimu wake.

Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Bw. Thomas Nade wakati akijibu hoja zilizowasilishwa na Waratibu wa Anwani za Makazi Taifa na Wilaya waliofika ofisini kwake tarehe 26 Agosti, 2024 kutoa mrejesho wa zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi wilayani humo.

Bw. Nade ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa TASAF Wilaya ya Ngorongoro, amesema kutokana na umuhimu wa elimu, miundombinu na mfumo wenyewe wa Anwani za Makazi, atahakikisha analifikisha kwenye vikao vya maamuzi ili katika robo ya pili ya mwaka wa fedha itengewe kiasi fulani.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya zoezi hilo kimkoa, Mratibu wa Anwani za Makazi Taifa, Mhandisi Jampyon Mbugi amesema licha ya zoezi la uhakiki, usasishaji na usajili kwenda vizuri bado upo umuhimu mkubwa wa Idara za Kisekta kuwashirikisha waratibu wa NaPA kwa kuwa sasa ni zoezi endelevu.

Awali waratibu hao walitembelea Ofisi ya Mtendaji Kata ya Engurosambu Kijiji cha Engurosambu kukagua maendeleo ya Uhakiki ambapo changamoto iliyoainishwa na watendaji hao wa Kata, Kijiji na Mtaa ni upatikanaji wa mtandao na umbali wa boma moja hadi nyingine inayochangiwa na jiografia ya eneo hilo.

Naye Bw. Jasson Kalile, Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na ambaye anasimamia Kata mbili ikiwemo ya Engurosambu katika zoezi hilo, amesema hadi kufikia tarehe 26 Agosti zaidi ya asilimia 70 ya Anwani zilikuwa zimesasishwa.
Waratibu wa Anwani za Makazi Taifa kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na wa Wilaya walipokutana na Mtendaji wa Kata ya Enguserosambu, Kijiji cha Engurosambu na Mtaa wa Engurosambu Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Arusha tarehe 26 Agosti 2024, ili kukagua maendeleo ya zoezi la Uhakiki wa Anwani za Makazi, Usasishaji na usajili wa taarifa za Anwani za Makazi tangu lililopozinduliwa siku ya tarehe 14 Agosti, 2024 katika Mkoa wa Arusha.

Kata hiyo ni miongoni mwa Kata mbili  za Ngorongoro zilizo mpakani mwa Kenya na Tanzania zenye changamoto ya eneo kubwa na mwingiliano wa wananchi wa nchi jirani ya Kenya pamoja na mawasiliano duni ya mtandao wa simu na intaneti.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: