Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Mwanza.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imetoa ruzuku ya sh. Milioni 135, kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania zaidi ya 30,000 katika Visiwa vitano vya Ziwa Viktoria vilivyoko Wilaya ya Sengerema kupata huduma za Mawasiliano.
Mnara huo uliojengwa katika Kisiwa cha Lyakanyasi Kijiji cha Chifunfu umelenga kutatua tatizo la kukosa mawasiliano hasa nyakati za majanga kama kuzama Ziwani, kutekwa na kupata majanga mengine bila kupata msaada wa haraka kutokana na kukosekana kwa mawasiliano.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) wakati akizungumza na wanakijiji wa Kisiwa cha Lyakanyasi Kata ya Chifunfu akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kukagua mradi ya ujenzi wa Mnara mikoa ya Kanda ya Ziwa.
"Mbali na wakazi wa visiwa vitano alivyovitaja Mbunge, mnara huu utawanufaisha watu zaidi ya 30,000, wa Kata ya Chifunfu Pia utawanufaisha wakazi 3,200 wa Kisiwa cha Chitandere na wapitaji hapa Visiwani, kwa hiyo watanufaika wengi zaidi," amesema Waziri Nape.
Amesema, Watanzania watakaonufaika na mnara huo wa Mawasiliano mbali na Lyakanyasi ni wa Visiwa vya Viswa, Biswa, Nyazune na Bihilai Wilaya ya Sengerema.
"Mnara huu ni unauwezo mkubwa, ni mnara wenye uwezo wa teknolojia ya 2G, 3G na 4G, mkiwa hapa mnaweza kutuma na kupokea fedha, kupigiana simu, kutumiana picha, kurekodi vedio na kuzituma, pamoja na kupakua video vizuri kama mko mjini," amesema na kusisitiza"
"Kwa hiyo ndugu zangu mnara huu tunategemea utakuwa chanzo cha mabadiliko makubwa ya maendeleo kwenye kisiwa chenu, mbali na watu kujiajiri katika huduma za uwakala, utaondoa tabia ya watu kuweka hela ndani na sasa wataweka kwenye simu zao."
Waziri Nape pia amewataka wananchi wa Visiwa hivyo kuutunza mnara huo uliojengwa na Kampuni ya Vodacom baada ya kupata ruzuku hiyo ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
Mnara huo uliwashwa tarehe 30 Juni, 2024 na Kampuni ya Vodacom na tayari umeanza kutoa huduma za Mawasiliano kwa wananchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments: