Dar es Salaam. Tarehe 11 Julai 2024: Akizindua msimu wa pili wa kipindi maalum cha televisheni cha elimu ya fedha kwa umma cha zogo mchongo kinachoandaliwa na Benki ya CRDB, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesifu jitihada hizo zinazolenga kuwakomboa wananchi kiuchumi hali itakayowasaidia kuondokana na umasikini.

Msigwa amesema elimu ya fedha itakayotolewa katika kipindi hiki cha Zogo Mchongo kupitia televisheni ya Clouds, itawafungua Watanzania wengi juu ya fursa zilizopo kwenye taasisi za fedha zikiongozwa na Benki ya CRDB. Maarifa watakayoyapata pia yatawasaidia kujikomboa kiuchumi na kuliwezesha taifa kuyafikia malengo ya kuwa na uchumi jumuishi,” amesema Msigwa.

Katibu mkuu huyo amesema kipindi hicho cha elimu ya fedha pia kinakwenda kusaidia kupambana na maadui wawili kati ya watatu waliotajwa na Mwalimu Nyerere ambao ni ujinga na umasikini na hilo likifanyika rahisi jamii kukabiliana na magonjwa. “Ukishapambana na ujinga na umasikini ni rahisi kutafuta maarifa mengine yakiwamo ya kukabiliana na maradhi,” amesema Msigwa.

“Nawapongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zenu za kuwaelimisha Watanzania. Kila mmoja akishiriki katika hili itakuwa rahisi kufanikisha malengo ya serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maisha ya Watanzania,” amesema Msigwa.

Aidha, Msigwa amesema kuwa fedha nyingi nchini zinazunguka kwenye sekta isiyo rasmi kwasababu wananchi wengi hawafahamu faida za matumizi ya huduma za benki. Kutokana na hivyo, Wajasiriamali wengi wamekuwa wakijinyima fursa za kunufaika na mikopo pamoja na huduma nyingine za benki.

“Ni imani yangu kipindi hiki cha Zongo Mchongo kitawafungua macho na kuwawezesha kuchangamkia fursa zitakazosaidia kukuza biashara zao na uchumi wa taifa letu,” ameongezea Msigwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kipindi hicho cha Zogo Mchongo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Elimu ya Fedha (2021/22 – 2025/26) unaolenga kuongeza ufahamu na matumizi ya huduma za fedha kwa wananchi.

Mbali na hayo, Nsekela alibainisha kuwa Zogo Mchongo imekuwa jukwaa muhimu la kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na akaunti za benki, kuwekeza, na kutumia huduma za kifedha kwa usalama na ufanisi. Hii ni hatua muhimu katika kufikia malengo ya kujumuisha kifedha na kuimarisha uchumi wa taifa kwa ujumla.

“Tukiwa Benki kiongozi ya kizalendo tunawajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya fedha kwani kwa kufanya hivyo sio tu tunasaidia kuchochea ujumuishi wa kifedha bali pia wa kiuchumi kwani elimu hii itasaidia watu kuchangamkia fursa za kiuchumi kutokana na maarifa waliyonayo ya huduma za fedha ambazo zinatolewa na Benki yao ya CRDB,” amesema Nsekela.

Nsekela aliongeza kuwa kupitia programu mbalimbali za elimu na uwezeshaji kwa jamii, Benki ya CRDB inaendelea kujitolea katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia watu wengi zaidi, hususan wale wa vijijini na maeneo yasiyo na huduma za benki.

Joseline Kamuhanda, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki ya CRDB, amesema kuwa msimu wa kwanza wa Zogo Mchongo ulikuwa na mafanikio makubwa, na kutokana na mafanikio hayo, wamefanya maboresho makubwa ili kurahisisha uelewa kwa watazamaji wa kipindi hiki kinachorushwa na Clouds TV.

"Msimu huu mpya tumeongeza mada nyingi ambazo zinaelimisha na kuburudisha. Tunataka watazamaji wetu wapate maarifa ya kina kuhusu masuala ya kifedha na waweze kujenga uelewa mzuri zaidi wa jinsi ya kudhibiti na kuwekeza fedha zao. Maboresho haya ni sehemu ya dhamira yetu ya kuendelea kuwahudumia wateja wetu na jamii kwa ujumla." amesema Joseline.

Kipindi cha Zogo Mchongo kinalenga kuongeza ufahamu wa masuala muhimu kama vile bajeti, utunzaji akiba, na namna ya kufanya uwekezaji. Mada zilizoongezwa ni katika msimu huu wa Zogo Mchongo ni pamoja na programu ya IMBEJU ambayo imekuwa kimbilio la vijana na wanawake wajasiriamali kote nchini, bidhaa kama Hodari kwa wajasiriamali, Huduma zinazofuta misingi ya sharia ‘Al Barakah’, huduma za Watanzania waishio nje ya nchi ‘Diaspora’, na uwezeshaji kwa biashara.



Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: