Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha.

Vikao vya Kamati za Ufundi vya Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) vimeendelea katika siku ya tatu jijini Arusha, ambapo Tanzania imewasilisha hoja zake mbalimbali ikiwemo kupendekeza kuwa na Mwakilishi kiongozi katika nafasi ya juu ya uongozi wa Umoja huo.

Hoja hiyo imetolewa na wawakilishi hao ikizingatiwa kuwa mkataba wa nchi mwenyeji inatakiwa kuchangia asilimia 50 ya bajeti ya uendeshaji ya PAPU kila mwanzo wa mwaka wa fedha iwapo nchi wanachama hazijachangia kwa wakati, fedha ambazo baadaye hurejeshwa.
Pendekezo hilo limetolewa leo tarehe 05 Juni, 2024 na wawakilishi wa Tanzania katika Kamati ya Fedha na Utawala kwenye Vikao vya Wataalam wa masuala ya Posta vinavyoshirikisha wajumbe kutoka mataifa 46 wanachama wa PAPU.

Aidha, wajumbe hao katika hoja zao wamesisitiza kuipata nafasi hiyo ili kuhakikisha usimamizi imara wa fedha zinazotolewa ambazo Tanzania imekuwa ikilipa kama nchi mwenyeji na pia kusimamia kikamilifu ili kupata marejesho ya gharama za ujenzi ilizolipa zaidi ya kiwango chao cha umiliki cha asilimia 40 (40%).
Kwa upande wa Kamati ya Mkakati (Strategy), wajumbe walionesha mchango mkubwa wa Tanzania katika ujenzi wa jengo la PAPU lililo Jijini, Arusha ambapo mwaka huu Mkutano wa 42 wa Baraza la Umoja wa Posta Afrika unafanyika.

Kamati hii imefikia maazimio ya kuunda Kikosi kazi katika Kamati ya Mkakati kitakachoshughulikia Upanuzi na Ushirikishaji watoa huduma katika Sekta ya Posta ambapo Tanzania imejitolea kushiriki pamoja na nchi za Botswana, Burkina Faso, Cameroon, DRC, Ivory Coast, Kenya, Misri, Namibia, Niger, na Uganda.
Wajumbe hao pia wamejadili masuala ya mapato na matumizi ya umoja, miradi, ajira na stahiki za watumishi wazawa, michango ya ada za uanachama na Mpango Mkakati wa miaka minne wa sekta ya Posta barani Afrika ili iweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: