Benki ya CRDB kupitia taasisi yake ya CRDB Bank Foundation, leo imezindua rasmi msimu wa nne wa mbio za CRDB Bank Marathon ikwa na lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya kusaidia kuboresha afya ya mama na mtoto nchini. Uzinduzi huo umefanyika wakati wa mahojiano ya wanahabari na Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mheshimiwa Mariam Mwinyi, yaliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar.

Akizindua msimu wa nne wa CRDB Marathon 2023, Mama Mariam Mwinyi aliipongeza Benki ya CRDB kwa msaada wake usioyumba kwa afya ya mama na mtoto kupitia mbio hizo. Katika hotuba yake, alitoa wito kwa Watanzania kutoka nyanja mbalimbali, pamoja na wakimbiaji kutoka nje ya Tanzania, kujiandikisha kwa wingi katika mbio za CRDB Bank Marathon 2023.
Mama Mariam Mwinyi alisisitiza kuwa juhudi za pamoja za washirika na wakimbiaji ni muhimu katika kufikia lengo la kuchangisha fedha kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili jamii ziilizoanishwa katika malengo ya mbio hizi ikiwamo afaya ya mama na mtoto. Aliongezea kuwa kumsaidia mama ni kusaidia jamii nzima na akawataka watu binafsi kuunga mkono jitihada hizo na kuchangia katika mbio hizo.

Katika mahojiano hayo Mama Mariam Mwinyi alizungumzia wito wake binafsi katika kusaidia jamii uliopelekea kuanzisha taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation yenye lengo la kuboresha maisha ya Wazanzibari kiuchumi na kijamii kwa kuzingatia zaidi afya ya mama na mtoto. Alitoa shukurani zake kwa benki hiyo kwa kuchagua kujikita katika sekta ya afya Zanzibar, eneo ambalo linamgusa sana na ambapo pia ni mdau mkubwa.
“Ustawi wa jamii yetu unahitaji kila mmoja wetu kuwa na wito wa kujitoa katika masuala mbalimbali ya kijamii,” alisema Mama Mariam Mwinyi. “Kupitia Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation tunalenga kuinua maisha ya Wazanzibari kiuchumi na kijamii kwa kutilia mkazo zaidi afya ya mama na mtoto, naipongeza Benki ya CRDB na washirika wake kwa kuungana nasi katika kuleta mabadiliko katika sekta ya afya Zanzibar kupitia CRDB Bank Marathon."

Mheshimiwa alitumia fursa hiyo pia kutangaza kuwa Mheshimiwa Dk Hussein Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, amekubali kuwa Mgeni Rasmi katika msimu wa nnne wa CRDB Marathon 2023. Mbio hizo zimepangwa kufanyika Agosti 13 katika viwanja vya The Green maarufu kama viwanja vya Farasi vilivyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Tully Esther Mwambapa, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya CRDB Bank Foundation, alieleza kuwa wamejipanga vilivyo kuhakikisha msimu wa nne unakuwa wa kipekee na uzoefu uliobora zaidi kwa wakimbiaji na washiriki wote. Tully anibainisha kuwa mbio za mwaka huu wamejipanga kuhakikisha usalama zaidi kwa wakimbiaji, na kusema kuwa katika upande wa burudani pia wamejipanga vilivyo na kuhimiza washiriki kujisajili wao pamoja na familia zao kwani mbio hizo pia zimezingatia burudani kwa watoto.

Mwambapa alibainisha kuwa msimu wa nne wa CRDB Bank Marathon unalenga kufikia malengo matatu muhimu. Kwanza, ujenzi wa kituo cha afya cha mama na watoto katika visiwa vya Zanzibar ni kipaumbele kikubwa. Mpango huo unaoendana na malengo ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, inayoongozwa na Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi, unaimarisha zaidi dhamira ya Benki ya CRDB katika kusaidia afya ya mama na mtoto nchini.
Pili, kupitia mbio hizo Benki ya CRDB imejipanga kuendeleza jitihada za kusaidia matibabu ya akina mama walio na mimba hatarishi na kutatua changamoto ya fistula katika hospitali ya CCBRT. Mwambapa alisisitiza umuhimu wamsaada huo sio tu kutoa matibabu bali pia kuwawezesha akina mama hao kiuchumi ili kusaidia familia na jamii zao ipasavyo.

Aidha, CRDB Bank Marathon 2023 inalenga kuendeleza msaada wake kwa matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Mwambapa amesema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita bado ipo ya haja ya kuendelea kushughulikia changamoto hiyo ya kiafya inayowaathiri watoto nchini.
Tullo Mafuru, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Sanlam ambao ni washirika wakubwa wa CRDB Bank Marathon amesema taasisi yao inajivunia kuwa sehemu ya mbio hizo kwa misimu minne mfululizo. Tullo alisema Sanlam ikiwa kampuni inayoongoza katika sekta ya bima nchini afya ya wateja imekuwa kipaumbele kikibwa kwao, sababu ambayo imepelekea kusaidia kufanikisha malengo ya mbio hizo husasani katika kusaidia afya ya mama na mtoto.

Usajili wa mbio za CRDB Bank Marathon 2023 umefunguliwa rasmi kupitia tovuti rasmi ya mbio hizo www.crdbbankmarathon.com. Watanzania na washiriki wa kimataifa wanakaribishwa kujisajili na kushiriki mbio hizi za kizalendo zenye nia ya kuboresha ustawi wa jamii nchini ikiwamo afya ya mama na mtoto nchini Tanzania. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, mwaka huu malengo ni kupata washiriki 7,000.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita mbio za CRDB Bank Marathon zimekua kwa kiasi kikubwa kwa, shukrani kwa washirika na wakimbiaji kutoka Tanzania na kutoka duniani kote. Kwa muda wa miaka mitatu iliyopita, mbio hizo zimeweza kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 1.5 kusaidia changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.

“Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kusaidia upasuaji wa watoto zaidi ya 300 wenye matatizo ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kusaidia ujenzi wa Kituo cha kisasa cha Mawasiliano katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, kusaidia matibabu ya akina mama walio katika mazingira hatarishi.
wajawazito katika Hospitali ya CCBRT,” alisema Mwambapa huku akiongeza kuwa fedha hizo pia zilisaidia uhifadhi wa mazingira kupitia kampeni ya Benki ya CRDB ya Pendezesha Tanzania, na Resi za Ngalawa wakati wa tamasha la Kizimkazi.

Mbio za CRDB Bank Marathon zimepata heshima kubwa kupelekea kupata usajili wa kimataifa kutoka kwa kutoka Chama cha Usajili na Upimaji wa Mbio za Kimataifa (AIMS) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Riadha (World Athletics).
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: