Na Mwadishi Wetu - Kajunason

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia( COSTECH)Dk.Amos Nungu amesema pamoja na Serikali na wadau kuendelea kutoa fedha za kufadhili utafiti na ubunifu nchini, kwa ujumla bado mahitaji ya kuratibu na kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu ni mengi ukilinganisha na rasilimali fedha zinazopatikana.

Akizungumza leo Juni 14, 2023/wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Nane la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ambapo amewaeleza washiriki pamoja na kufadhili watafiti kufanya tafiti mbalimbali bado mahitaji ni mengi ukilinganisha na rasilimali fedha.

Amesema kuwa changamoto hiyo ya fedha inachangia taasisi nyingi za utafiti na maendeleo, pamoja na vyuo vikuu kushindwa kufanya tafiti na bunifu nyingi zaidi zitakazoleta mapinduzi makubwa ya kijamii na kiuchumi.

Pamoja na changamoto hiyo ya rasilimali fedha, ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa katika kuratibu, kukuza na kuendeleza utafiti; Tume huratibu maandalizi ya vipaumbele vya utafiti kulingana na vipaumbele vya taifa.

"Kwa sasa, upo Mwongozo wa Vipaumbele vya Kitaifa vya Utafiti vya miaka mitano yaani, mwaka 2021/22 hadi mwaka 2025/26 ambao unatumika kufadhili tafiti na pia kuwaongoza wadau wengine wanaotaka kufadhili au kuwekeza katika utafiti.

"Kwa kipindi cha miaka mitano (2018-2023 Serikali kupitia Tume imefadhili miradi 47 ya utafiti yenye thamani ya takribani Sh. billion 5 fedha za kitanzania. Katika kipindi hicho cha 2018-2023, pia Tume imefadhili miradi 11 ya miundombinu ya Utafiti yenye thamani ya zaidi ya billion 4 ya fedha za kitanzania.

"Tume imewezesha watafiti wa ndani na nje ya nchi kufanya tafiti hapa nchini kwa kuratibu utoaji wa vibali vya utafiti. Katika baadhi ya maombi ya vibali vya tafiti, Tume hushirikisha wadau wa sekta husika ili wafahamu utafiti gani unaendelea, wajiandae kupokea matokeo ya tafiti hizo yaweze kutumika na Serikali, " amesema Dk.Nungu.

Aidha katika kuendeleza na kuhawilisha teknolojia na ubunifu amesema Tume inafanya kazi kwa karibu na wabunifu walioko katika sekta rasmi na isiyo rasmi na kwamba wamekuwa wakitumia njia tatu katika kuwaendeleza wabunifu.

Ametaja njia hizo ni kutoa ushauri wa kitaalamu moja kwa moja au kupitia wabobezi wanaopatikana hapa nchini, kuwaunganisha na taasisi bobezi ili kuwapa usaidizi stahiki kulingana na aina ya ubunifu wao.

Ameongeza baadhi ya wabunifu wameunganishwa na Watanzania wabobezi walioko nje ya nchi (Diaspora) kwa ajili ya ushauri pamoja na kuwapa usaidizi wa kifedha (mwega), ambao ni uwekezaji kama wa mbegu tu ili waendeleze bunifu zao.

"Ili kuhakikisha wabunifu wengi zaidi wanafikiwa, Tume iliandaa “Mwongozo wa Kitaifa wa kutambua na kuendeleza ugunduzi, ubunifu na maarifa asilia ambao ulipitishwa na Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknilojia mwaka 2018 uliopelekea kuanzishwa Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) mwaka 2019.

"Hadi kufikia sasa, zaidi ya wabunifu 2,647 wametambuliwa na kupata usaidizi. Wabunifu 461 kati ya wale waliotambuliwa walikidhi vigezo vya kupata usaidizi wa fedha na hivyo wamepatiwa mwega wa kuendeleza bunifu zao, " amesema.

Aidha Dk.Nungu amesema moja ya miradi ya kujivunia iliyotokana na MAKISATU ni Mradi wa Dira za Maji za malipo kabla ya matumzi (prepaid water meters) ambao ulibuniwa na kijana aliyekuwa anasoma diploma na kwa sasa Mamlaka ya Maji na Usafi Vijijini (RUWASA) wametoa nafasi mita hizi zifungwe mikoa yote ya Tanzania Bara.

Ameeleza kwamba katika kila Mkoa Wilaya mbili zitachaguliwa na kufungiwa mita 8 kila moja na tayari mita zaidi ya 30 zimefungwa huku matazamio ni kwamba hadi mwishoni mwa Julai mita 4 kila Wilaya za mikoa yote Tanzania Bara zitakuwa zimefungwa.

"Tume inafanya kazi kwa karibu na taasisi zinazojihusisha na uendelezaji na uhawilishaji wa teknolojia. Kwa namna mbalimbali, Tume inaziwezesha taasisi hizi kwa kuzipatia fedha za kufadhili miradi ya ubunifu; kujengea uwezo watumishi wao, na pia kuboresha miundimbinu ya taasisi hizo.

"Taasisi hizi zimekuwa ni nyenzo muhimu za kusanifu na kutengeneza mashine mbalimbali ambazo zinawasaidia wananchi hususani katika sekta ya kilimo, mifugo, afya na uzalishaji. Pia taasisi hizi pamoja na vyuo vikuu zimekuwa ni nyenzo muhimu za kulea na kukuza vipaji vya wabunifu hapa nchini, " amesema.

Katika hatua nyingine alisema Tume kwa kushikirikiana na taasisi mbalimbali pamoja na vyuo vikuu vya hapa nchini, imewezesha wabunifu kuanzisha kampuni yanayotokana na ubunifu (startup companies) kwa kuboresha bidhaa au huduma.


Amesema kampuni hizo zimetengeneza zaidi ya ajira 1,800 za moja kwa moja na 3,000 zisizo za moja kwa moja ambapo kampuni kama vile Intemech, Magilah Tech, Scan code (T) Limited, Sahara Ventures, Nanofilter, zimeweza kubiasharisha ubunifu waao, kuwa na masoko hadi nje ya mipaka ya nchi yetu.

Amesema kwamba tayari Tanzania kwa sasa inauza hizo teknolojia nje ya nchi kama vile Malawi, Zambia, Afrika Kusini, na kwingineko.




Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: