Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV - Dodoma
Serikali imesema kuwa uchunguzi wa ajali ya Ndege ya Precision Air iliyotokea Novemba 6, mwaka huu unaendelea na ulianza tangu siku ya kwanza ilipotokea ajali hiyo katika Ziwa Victoria mjini Bukoba mkoani Kagera.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kuwa Baraza la Mawaziri lililokutana leo (Novemba 14, 2022) limeagiza uchunguzi wa ajali hiyo ufanyike baina na Wataalamu wa ndani kwa kushirikiana na Waatalamu kutoka nje ya nchi ili kutoa taarifa ya chanzo chake.
“Nchi yetu imetiliana saini za makubaliano katika mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo inasimamia usafiri wa Anga, na hivyo kuhakikisha hatua stahiki zitachukuliwa baada ya ajali za Ndege kutokea”, amesema Msigwa baada ya Baraza la Mawaziri kutoa tamko.
Aidha, Msigwa amesema Baraza hilo la Mawaziri limeagiza kuimarishwa Vitengo vyote vinavyokabiliana na majanga nchini ili kuchukua tahadhari dhidi ya ajali kama hiyo iliyosababisha idadi kubwa ya vifo vya watu.
Msigwa amesema timu hiyo ya uchunguzi kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka nje, itatoa ripoti ya awali ya ajali hiyo katika siku 14, pia itatoa ripoti ya ajali hiyo ndani ya siku 30 na mwisho itatoa ripoti ndani ya miezi 12 baada ya ajali kutokea.
Serikali imewataka Wananchi kuwa na utulivu katika kipindi cha uchunguzi wa ajali hiyo, huku ikiwahakikishia Wananchi kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inachukua tahadhari na kuzuia ajali na majanga mbalimbali yanayotokea nchini
Ajali ya Ndege ya Kampuni ya Precision Air ilitokea Jumapili ya Novemba 6, 2022 katika Ziwa Victoria, ilibeba watu 43 ambapo ilisababisha vifo vya watu 19 wakiwemo Marubani wawili na wengine 24 kujeruhiwa kati ya majeruhi hao Wahudumu wa Ndege hiyo walikuwa wawili.
Toa Maoni Yako:
0 comments: