Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewafungulia milango muhimu vijana wabunifu katika Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuwapa uwezeshaji uliokuwa unakwamisha ubunifu miaka yote nchini.
TCRA kwa ushirikiano na taasisi nyingine, imeweka mazingira rafiki kwa vijana wabunifu wa TEHAMA kutengeneza fursa za kukuza ubunifu na hatimaye kuzaa ajira kwa vijana. Fursa zilizotolewa zinahitaji kijana kuwa na ubunifu kama mtaji wake na vifaa vya gharama nafuu vya TEHAMA kama vile kompyuta mpakato na simu ya kiganjani au vifaa rununu pendwa kama vile kishikwambi kukamilisha ubunifu wake.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari amesema Serikali ya Tanzania imeamua kutoka rasilimali kwa vijana wabunifu katika sekta ya TEHAMA. Rasilimali za mawasiliano zinazotolewa na TCRA kwa ajili ya vijana wabunifu kufanya majaribio ni pamoja na misimbo ya USSD, yaani rasilimali-namba. Hizi ni namba maalum zinazotumika kumpa mbunifu fursa ya kusambaza teknolojia aliyoibuni ndani na nje ya nchi.
Pia TCRA kwa sasa wanato kikoa (domain) cha dot tz (.tz) na masafa ya mawasiliano. Kuanzia mwaka 2021, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir (Pichani juu), amesisitiza kuwa vijana wabunifu na wavumbuzi wa programu mbalimbali za kidijitali sasa wanaweza kujitokeza kupata rasilimali hizo zitakazowawezesha kupata fursa ya kutengeneza ajira; kujiletea kipato na kutatua changamoto mtambuka za jamii.
“Tumejipanga kuhakikisha wabunifu wapya hasa wa sekta ya TEHAMA, wanaoweza kutatua changamoto za jamii yetu wanapata rasilimali hizi za mawasiliano, ili washiriki katika uchumi wa kidijiti,” amesisitiza Mkurugenzi Mkuu Dk. Jabir.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeondoa malipo ya ada ya maombi na usajili wa leseni wa rasilimali hizo kwa ajili ya wabunifu wenye nia ya kubuni suala lolote litakalorahisisha mazingira ya kawaida ya kila siku ya mwananchi. Wabunifu wanaotaka kutumia fursa hii wanaweza kuwasiliana na Dawati la Huduma la TCRA kupitia namba 0800008272 au kutembelea tovuti www.tcra.go.t.
Toa Maoni Yako:
0 comments: