Na Mwandishi Wetu
SHULE ya Msingi Hazina ya Magomeni jijini Dar es Salaam, imeongoza kwenye matokeo ya mtihani wa utamilifu (Mock), darasa la saba kwa Wilaya ya Kinondoni.
Kwenye matokeo hayo yaliyotolewa na Mkoa wa Dar es Salaam, hivi karibuni, shule hiyo imeshika nafasi ya kwanza kati ya shule 158 za wilaya hiyo.
Mkuu wa shule hiyo, Omar Juma, alisema jana kuwa shule hiyo iliongoza kwenye mtihani uliofanyika mwezi wa nne na ule uliofanyika mwezi wa saba mwaka huu.
Alisema walimu wake wamekuwa wakijituma kuwaandaa wanafunzi hao kwaajili ya mitihani ya ndani na ile ya kitaifa na kwamba hiyo ndiyo imekuwa siri kubwa ya mafanikio kwao.
Alisema kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya kwa wanafunzi hao wanaimani kwamba watafanya vizuri zaidi pia kwenye mtihani wa kitaifa wa darasa la saba mwaka huu.
“Sisi tunapiga kazi hapa ni kazi tu nawashukuru walimu kwa kuifanya shule hii kuongoza mtihani wa utamilifu kwa mara ya pili mfululizo hii inatupa moyo wa kuendelea kufanyakazi,” alisema Omar
Alisema kujituma kwa walimu na ushirikiano ambao wamekuwa wakiupata kwa uongozi wa shule na wanafunzi ndiyo kitu wanachojivunia.
“Walimu wanafanyakazi kwa moyo sana, wazazi wa wanafunzi wamekuwa wakitoa ushirikiano mzuri sana kwa shule na uongozi wa shule unawajali sana walimu, hayo kwa pamoja yamekuwa yakisaidia ufaulu wetu kuwa juu mwaka hadi mwaka,” alisema
Aliwapongeza wanafunzi kwa mafanikio hayo na kuwataka wasome kwa bidii ili hatimaye waweze kuendelea kuongoza kitaifa na Mkoa wa Dar es Salaam kwenye mitihani ijayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: