WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso pamoja na Naibu Waziri wa Maji Maryprisca Mahundi wameongoza Menejimenti ya Wizara ya Maji kwa kukutana na Ujumbe wa Sekretariati ya Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika (LTA) yenye Makao Makuu Jijini Bujumbura, Burundi katika ukumbi wa wizara, Mtumba.
Ujumbe huo uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa LTA Sylvain Tusanga pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, DkJilly Maleko. Aidha Sekretariati ya Bonde la Ziwa Tanganyika ndio inasimamia shughuli za kila siku za Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika (Convention on Sustainable Management of Lake Tanganyika) ambao uliwekwa saini na nchi wanachama tarehe 12 Juni 2003 Jijini Dar es Salaam. Nchi wanachama wa LTA ni Burundi, DRC, Tanzania na Zambia.
Lengo la ziara ya Sekretariati ya LTA ilikuwa ni kuelezea hatua zilizofikiwa katika utayarishaji unaojulikana kama Lake Tanganyika Integrated Regional Development Programme (PRODAP) Awamu ya Pili, baada ya Awamu ya Kwanza ya mradi huo, unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika, kukamilika kwa mafanikio.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari imeeleza katika ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa LTA ameiomba Wizara ya Maji kuwasilisha vipaumbele vyake ili viweze kuzingatiwa wakati huu wa maandalizi ya Awamu ya Pili ya Mradi wa PRODAP.
Pia aliezea Mradi mwingine unaotekelezwa na LTA unaojulikana kama Lake Tanganyika Water Management (LATAWAMA). Mradi unajihusisha na kuhakikisha kwamba rasilimaliza maji zinasimamiwa na kutumika kwa uendelevu na pia kuzuia uchafuzi wa rasilimali hizo.
Katika majadiliano, Waziri wa Maji, amesisitiza kuwa LTA iwe sasa ni suluhu ya matatizo ya maji kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Tanganyika.
Wananchi wengi katika maeneo ya pembezoni mwa ziwa hilo hawana huduma za maji safi na salama na pia hawana huduma za usafi wa mazingira na kusababisha uchafuzi wa rasilimali za maji katika Ziwa hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: