Na Adeladius Makwega-WUSM Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini ndugu Saidi Yakubu amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ana imani kubwa na watumishi wa umma la msingi kwa kila mmoja anapashwa kufanya kazi kwa bidiii na maarifa ili kuliendeleza taifa letu la Tanzania.
Kauli hiyo ya Naibu Katibu Mkuu Yakubu ameitoa Februari 10, 2022 wakati anazungumza na maafisa kadhaa wa wizara hii Mtumba Mji wa Selikali jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya vikao na watumishi wa wizara hii tangu ateuliwe mwezi mmoja uliopita.
“Watumishi wa umma tunapaswa kuwa wawazi na wakweli kwa serikali yetu katika vipindi vyote tunavyohudumu, maana maisha yetu yanategemea serikali kwani tunalipwa ujira kwa kazi hizi tunazozifanya.”
Naibu Katibu Mkuu Yakubu aliongeza kuwa mpaka sasa ameona watumishi wanafanya kazi kwa kujituma sana hadi saa za ziada. Aliwapa hongera watumishi hao huku akibainisha maeneo machache yanayotakiwa kuboreshwa.
“Changamoto zote ninazipokea, nitazifanyia kazi nikishirikiana viongozi wenzangu wakiwamo Katibu Mkuu, Naibu Waziri na Waziri wetu mara baada ya kutoka tu katika kikao hiki.”
Awali Naibu Katibu Mkuu huyo alitoa nafasi kwa maafisa wa wizara hii kueleza changamoto kadhaa walizonazo. Wakizitaja changamoto hizo kwa uhuru wote walisema kuwa wana uhaba wa vitendea kazi mathalani magari na kompyuta, maboresho ya stahiki mbalimbali na kutolewa kwa fursa sawa kwa wote.
Kikao hicho cha Naibu Katibu Mkuu Saidi Yakubu na maafisa wa wizara hii ni sehemu ya muendelezo ya vikao vya wizara hiyo vinavyofanyika na watumishi wizarani hapo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: