Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella na Afisa Mtendaji Mkuu wa ENGIE Energy Access wa Dunia, Gillian-Alexandre Huart wakizindua rasmi chapa ya umeme jua ya Mysol jijini Arusha mwishoni mwa wiki. Mysol inachukua nafasi ya Mobisol kufuatia kampuni ya ENGIE, mzalishaji mkuu huru wa umeme duniani kuzinunua kampuni mbili za nishati ya jua Mobisol na Fenix International ikiwa ni sehemu ya kupanua wigo wake barani Afrika.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha akitazama maonyesho ya bidhaa za umeme jua za Mysol jijini Arusha mwishoni mwa wiki baada ya kuzindua rasmi chapa hiyo. Kushoto kwake ni Afisa Mtendaji Mkuu wa ENGIE Energy Access wa Dunia, Gillian-Alexandre Huart
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella pamoja na Mkurugenzi wa Engie Mobisol Godfrey Mugambi (wa pili kushoto), msanii wa vichekesho na Mhamasishaji wa Mysol, Lucas Mhuvile “Joti” (wa tatu kushoto) pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa ENGIE Energy Access wa Dunia, Gillian-Alexandre Huart baada ya uzinduzi rasmi wa chapa ya MySol.

Na Mwandishi Wetu - Arusha

ENGIE Mobisol U.K Ltd, kampuni inayoongoza katika sekta ya nishati ya umeme jua kupitia mpango wa mikopo ya huduma za nishati wa lipa kadri unavyotumia (PAYGo) nchini Tanzania imetangaza mabadiliko ya chapa yake kuu ya kibiashara ya Mobisol kwenda MySol. Mabadiliko ya jina yanafuatia kampuni ya ENGIE, mzalishaji mkuu huru wa umeme duniani kuzinunua kampuni mbili za nishati ya jua Mobisol na Fenix ​​International na kama sehemu ya azma ya kupanua wigo wake barani Afrika.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na wadau wa sekta ya nishati, wakiwemo watendaji wa serikali, wadhibiti wa Sekta ya Nishati, Viongozi wa Viwanda, Fedha, Ufundi, Washirika wa Usambazaji na Wadau wengine wengi, Godfrey Mugambi, Mkurugenzi Mkuu wa ENGIE Mobisol aliwafahamisha waliohudhuria kuwa kampuni iko tayari si tu kuziba pengo la upatikanaji wa umeme nchini Tanzania, lakini pia kuchangia kikamilifu katika upanuzi wa usambazaji wa umeme kwenye maeneo yaliyoko nje ya gridi ya taifa.

“Mpaka sasa tumepata mafanikio makubwa kwa kuboresha maisha ya Watanzania zaidi ya 600,000 kutoka kaya Zaidi ya 120,000 na kutokana na uwekezaji huu tunayo mipango kabambe ya kuendelea kujitanua kwa kasi zaidi na kufikisha nishati yetu safi, ya uhakika na nafuu kwa mamilioni ya Watanzania katika kipindi cha miaka mitano ijayo”, alisema Mugambi.

Aliongeza kuwa ENGIE imedhamiria kutoa mchango unaoleta matokeo katika uchumi kwa kutoa huduma zinazochangia maendeleo katika sekta muhimu za uchumi ikiwemo kilimo kupitia pampu za gharama nafuu za nishati ya jua kwa ajili ya umwagiliaji pamoja na vifaa vya umeme jua kwa matumizi ya viwandani.

Imezinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella, hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ENGIE Energy Access Global Gillian-Alexandre Huart.

Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella alisema hatua hiyo ya uwekezaji inapaswa kusaidia juhudi za serikali katika kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo. "Tunatarajia kuongezeka kwa uwezo wa kutoa huduma za nishati katika maeneo yaliyopo nje ya gridi ya taifa.”

“Azma ya serikali ni kutoa huduma ya umeme kwa wote; kwa hivyo, hii ni fursa ya kuchukua mahitaji haya na kuunga mkono azma ya usambazaji wa umeme kwa kuendelea kuwekeza katika mpango wa nishati ya jua nje ya gridi ya taifa.

RC alipongeza mpango wa mikopo ya huduma za nishati wa PayGo ambao unasaidia kaya kwa kurahisisha malipo ya mifumo ya umeme jua ambapo ulipia taratibu huku wakiendelea kupata huduma. Alisema serikali pia inatambua mchango wa ENGIE kwenye katika uchumi kwa kutoa maelfu ya ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: