Wahasibu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kutoka kulia ni Stephen Swai (35), Mhasibu Msaidizi, Philip Sengela (43), Mhasibu Msaidizi, Ally Mwinyimvua (49), Mhasibu, Laurent Albert (33) Mhasibu Msaidizi na Mohamed Swalehe (22) Kibarua wakiwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mara baada ya kusomewa kesi yao ya uhujumu uchumi.
Karama Kenyunko Michuzi TV
WAHASIBU wanne wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Kibarua mmoja, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye shtaka moja la kuisababishia Bandari hasara ya zaidi ya Sh. Milioni 600.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Mwandamizi, Faraja George akisaidiana na Grace Mwanga imewataja washtakiwa hao kuwa ni, Stephen Swai (35), Mhasibu Msaidizi, Philip Sengela (43), Mhasibu Msaidizi, Ally Mwinyimvua (49), Mhasibu, Laurent Albert (33) Mhasibu Msaidizi na Mohamed Swalehe (22) Kibarua.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya imedaiwa kuwa kati ya Julai Mosi 2019 na Novemba 30, 2021 huko katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) iliyopo eneo la Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, washtakiwa walitenda kosa.
Inadaiwa, siku hiyo washtakiwa kwa makusudi waliingiza data za uongo kwenye mfumo wa malipo wa Bandari kitendo kilichoisababishia Bandari hiyo hasara ya Sh. 694,072,463.90
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida zinasikilizwa Mahakama Kuu.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado unaendelea na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 29,2021 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: